• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Nchi kukopa Sh929 bilioni

Nchi kukopa Sh929 bilioni

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI itakopa Sh2.5 bilioni kwa siku kwa kipindi cha miezi 12 ijayo ili kutekeleza bajeti yake ya Sh3.03 trilioni iliyosomwa jana Bungeni na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.

Kinaya ni kuwa Sh2.8 bilioni nazo zitatumika kila siku kulipa madeni yanayodaiwa Kenya na wadeni wa humu nchini na kimataifa.Kulingana na Waziri Yatani, bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 ina pengo la Sh929.7 bilioni, ambalo litajazwa kupitia mikopo kutoka mataifa ya kigeni na taasisi za kifedha za humu nchini.

Serikali itakopa Sh271.2 bilioni kutoka mataifa ya kigeni na Sh658.5 bilioni kutoka taasisi za kifedha za humu nchini.Sehemu kubwa ya bajeti, Sh1.2 trilioni nayo itatumika kulipa deni ambalo Kenya inadaiwa.

Hiyo inamaanisha kwamba kwa kila Sh100 zinazokusanywa na Mamlaka ya Ushuru (KRA), karibu Sh60 zitatumika kulipa madeni. Hii ina maana kuwa serikali itasalia na Sh30 kulipa mishahara na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Serikali inatarajia kupitia KRA kukusanya mapato ya Sh2.03 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 unaoanza Julai 1, mwaka huu.Kwa sasa Kenya inadaiwa jumla ya Sh7.4 trilioni, kulingana na takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Kufikia mwishoni mwa Juni mwaka ujao deni la kitaifa litakuwa zaidi ya Sh9 trilioni na kila Mkenya atakuwa anadaiwa Sh180,000.Kulingana na CBK, kufikia Machi, mwaka huu, Kenya ilikuwa ikidaiwa Sh3.6 trilioni na taasisi za kifedha za humu nchini na ShSh3.8 trilioni na mashirika ya kifedha ya kimataifa na nchi za kigeni kama vile China, Ufaransa, Italia, Japan, Uhuspania, Amerika, Ubeligiji, Canada, Denmark, Ujerumani na Korea Kusini.

Mnamo Oktoba 2019, Bunge liliruhusu serikali kuendelea kukopa hadi deni litakapofikia Sh9 trilioni.Tathmini ya Bajeti ya 2020 iliyofanywa na Wizara ya Fedha ilionyesha kuwa deni la kitaifa litafikia Sh9 trilioni katika mwaka ujao wa matumizi ya fedha wa 2022/2023.Lakini jana, Bw Yatani alilitaka Bunge kubadili sheria ili kuruhusu serikali kukopa zaidi katika mwaka wa fedha utakaoanza Julai 1, 2021.

Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti katika ripoti yake mapema wiki hii, ilipendekeza kuwa kiwango cha juu cha deni la kitaifa kinafaa kuongezwa ili kuwezesha serikali kukopa zaidi.Ripoti ya Kamati ya Bunge inasema kuwa serikali huenda ikakosa fedha za kuendesha miradi yake katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, endapo kiwango cha juu cha deni kitasalia Sh9 trilioni.

Ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti, Margaret Nyakang’o inaonyesha kuwa serikali ilikopa Sh1.06 trilioni kati ya Machi 2020 na Machi 2021.Ripoti hiyo inaonyesha kuwa serikali ilikopa wastani wa Sh2.89 bilioni kwa siku ndani ya kipindi hicho.

Rais Uhuru Kenyatta alirithi deni la Sh1.89 trilioni kutoka kwa serikali ya mtangulizi wake Mwai Kibaki. Ndani ya mwaka mmoja wa utawala wa Jubilee, deni liliongezeka hadi Sh2.37 na Sh4.4 trilioni mwishoni mwa muhula wa kwanza wa Rais Kenyatta.

Kwenye bajeti hiyo, serikali kuu imetengewa Sh1.89 trilioni, Bunge (Sh46.6 bilioni), Mahakama (Sh17.9 bilioni) na kaunti Sh370 bilioniBw Yatani alisema kuwa uchumi unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 6.6 mwaka huu: “Hii ni kutokana na mazingira mazuri ya kibiashara na shughuli ya kutoa chanjo ya ugonjwa wa corona ambao umetikisa uchumi.”

  • Tags

You can share this post!

Kilimo chatengewa Sh60b

Agizo la Magoha kuhusu karo linakiuka ahadi ya serikali