• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
TAHARIRI: Tumalize uhuni wa wanafunzi shuleni

TAHARIRI: Tumalize uhuni wa wanafunzi shuleni

Na MHARIRI

MIAKA michache iliyopita, serikaliilipotaka kuondoa adhabu ya viboko shuleni, tulionya kuwa hatua hiyo huenda ikawa na atharimbaya kwa mfumo wa nidhamu.

Wakati huo, wadau katika sekta ya elimu walionelea ilikuwa vyema kuwakanya watoto kwa nasaha, maneno mazuri na kuwabembeleza. Kwamba haki za watoto zinakataza hata mzazi kumwadhibu mwanawe kwa kiboko.

Haki hizo za watoto zilipigiwa debe baada ya kubainika kuwa kulikuwa na baadhi ya walimu waliowaadhibu watoto kwa kuwaumiza. Lengo la adhabu ni kutisha, kumfanya mkosaji ajute na asirudie kosa. Lengo si kumpiga kama nyoka au kumsababishia majeraha mwilini.

Kuna walimu ambao wamewahi hata kuwavunja mikono wanafunzi kutumia kiboko.Lakini makosa ya walimu wachache hayakuwa sababu ya kwenda kinyume na maandiko, kwamba mtoto aelekezwe kwa hekima lakini ikibidi, achapwe.

Kwa kuondoa kiboko na kuwapa watoto uhuru kupita kiasi, hali ya nidhamu ya Wakenya imekuwa duni. Tunakuwa na watu kwenye jamii walio na elimu ya hali ya juu lakini hawana hekima wala nidhamu.Matukio mengi yamedhihirisha jambo hili.

La punde zaidi ni kisa cha mwanafunzi wa shule ya upili ya Ainamoi Kaunti ya Kericho. Polisi wanamsaka kijana huyo, anayesemekana kumchapa Mwalimu mkuu kwa ubao uliokuwa na msumari.

Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alimvamia Bw Geoffrey Rono akiwa ofisini mwake mwendo wa saa kumi na mbili za jioni. Alitoroka na kumwacha Mwalimu mkuu huyo akivuja damu kichwani. Sababu hasa ya tukio hilo ni kwamba eti Bw Rono alikuwa ametekeleza tamko la waziri wa Elimu Prof George Magoha kuwataka wanafunzi waliokuwa wanadaiwa karo, waende nyumbani.

Hili si tukio la kwanza la Mwalimu kushambuliwa na wanafunzi. Kuna walimu kadhaa ambao mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu wameshambuliwa na wanafunzi.Matukio ya aina hii yalianza pale serikali na jamii walipomdunisha mwalimu.

Ingawa mwalimu anachukuliwa kibadala cha mzazi, jamii imemkosea heshima na kumnyima haki zote na heshima anazostahili.Ikiwa tunataka kurejesha nchi ilipokuwa miaka ya 80, ambapo mwalimu alikuwa mtu muhimu katika jamii, ni lazima tukabili kisa cha Kericho na vingine kama hivyo kwa ukali unaostahili.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki Nakuru kuona Safari Rally angani kwa ndege

Mukhisa Kituyi adaiwa kumdhulumu mwanamke kimapenzi