• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Hatari ya Sagana River Water Fall, Muruguru – Nyeri

Hatari ya Sagana River Water Fall, Muruguru – Nyeri

Na SAMMY WAWERU

MAZINGIRA ya mshuko wa maji ya Mto Sagana eneo la Muruguru, Kaunti ya Nyeri yangali yanazua wasiwasi kuhusu usalama wa wakazi na wageni wanaozuru eneo hilo.

Mshuko huo wa maji, maarufu kama Sagana River Water Fall, si mgeni katika vyombo vya habari kutokana na visa vya watu kufa maji.Wengi wa wanaoathirika ni wageni wanaozuru eneo hilo kutalii, na katika harakati za kupiga picha ili kunasa mshuko wa maji, endapo hawawi makini hujipata kuteleza na kuanguka humo.

“Visa vya watu kufa maji Sagana River Water Fall ambavyo tumeshuhudia ni vingi. Wanaoangukia humo wakati wakipiga picha hawanusuriki kifo,” Bw Charles Nderitu, mkazi akaambia Taifa Leo Dijitali.Ni matukio yanayoshuhudiwa mara kwa mara, hasa kwa wasiofahamu eneo hilo, wanaolizuru kwa mara ya kwanza.

“Si ajabu kuona wavulana wa eneo hili wakipiga mbizi katika vidimbwi vya mshuko huo na watoke salama. Wamefahamu vidimbwi vyenyewe na sehemu ambayo si salama, ila kwa wageni ni hatari,” Charles akaelezea.Mshuko huo wa maji hutumika kuzalisha nguvu za umeme, kupitia Sagana Power Station.

Novemba 2019, mwanafunzi mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Masuala ya Teknolojia cha Dedan Kimathi, Nyeri, alikufa maji wakati akiogelea katika kidimbwi cha mshuko huo, chenye kina cha urefu wa futi 70.Aidha, mshuko wa maji una urefu wa futi 100.

Mvua inaponyea, mawe ya mazingira huwa televu, suala ambalo ni hatari.Licha ya visa vya watu kuendelea kufa maji eneo hilo, hakuna hatua ambayo serikali imechukua kuimarisha usalama.

Picha/ Sammy Waweru.
Mshuko wa maji Mto Sagana eneo la Muruguru, Kaunti ya Nyeri.

“Tunaomba eneo la mshuko lizingirwe kwa ua. Eneo hili si salama,” akahimiza Shimba Njohe, mkazi.Isitoshe, eneo hilo linahitaji daraja bora kuunganisha Muruguru na Wakamata. Lililoko limeundwa kwa mbao, katika mto (Sagana) ambao hufurika na kuwa hatari.

 Picha/ Sammy Waweru.
Bw Shimba Njohe akielezea kuhusu hatari ya mshuko wa maji Mto Sagana eneo la Muruguru, Kaunti ya Nyeri.
  • Tags

You can share this post!

Mukhisa Kituyi adaiwa kumdhulumu mwanamke kimapenzi

Mkulima anavyochuma kwa mimea na ufugaji samaki