• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Spika ataka Yatani akamatwe kwa kukaidi seneti

Spika ataka Yatani akamatwe kwa kukaidi seneti

Na IBRAHIM ORUKO

SPIKA wa Seneti, Kenneth Lusaka sasa anataka Waziri wa Fedha Ukur Yatani akamatwe kwa kukaidi mialiko kadhaa ya kumtaka afike mbele ya maseneta.

Kulingana na Bw Lusaka, Waziri Yatani amekataa kufika mbele ya Kamati ya Seneti kutoa ufafanuzi kuhusu hatua ya serikali ya kitaifa kuchelewesha fedha za kaunti.

Huku zikiwa zimesalia siku 18 kabla ya mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021 kufikia mwisho, Juni 30, serikali za kaunti hazijapokea jumla ya Sh103.5 bilioni.

Baraza la Magavana (CoG) mara kwa mara limekuwa likishutumu serikali ya kitaifa kwa kuchelewa kuwasilisha mgao wa fedha kwa serikali za kaunti.

Katika barua yake kwa Waziri Yatani, Lusaka anashutumu Wizara ya Fedha kwa kutatiza ugatuzi.

“Katiba inataka waziri kufika mbele ya Kamati ya Bunge kutoa majibu kuhusiana na masuala mbalimbali kuhusiana na afisi yake,” akasema Bw Lusaka kupitia barua iliyoandikwa Juni 7, 2021.

Bw Yatani amepuuza mialiko mitatu ya kumtaka kufika mbele ya Kamati ya Seneti inayoongozwa na Seneta wa Kirinyaga, Charles Kibiru.

Waziri Yattani alialikwa kufika mbele ya kamati Mei 26, mwaka huu, lakini mkutano huo uliahirishwa hadi Juni 3. Lakini waziri hakufika –hatua iliyomfanya Bw Kibiru kupeleka malalamishi yake kwa spika.

Bw Lusaka amesema kuwa ataagiza kukamatwa kwa Bw Yatani iwapo atakosa kufika mbele ya Kamati ya Seneti iwapo atakaidi mwaliko wa kumtaka kufika binafsi mbele ya Kamati ya Seneti. Kikatiba, kamati za bunge zina mamlaka sawa na ya Mahakama na kukaidi mialiko ni sawa na kukaidi amri ya korti.

You can share this post!

Shabana waomba uungwaji mkono

FKF yafanikisha klabu 11 za Nairobi kupokea chanjo ya pili...