• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Miradi ya Uhuru Nyanza inavyotishia kuchimbia Raila kaburi la kisiasa

Miradi ya Uhuru Nyanza inavyotishia kuchimbia Raila kaburi la kisiasa

Na CHARLES WASONGA

ZIARA ya Rais Uhuru Kenyatta majuzi katika eneo la Luo Nyanza imegeuka shubiri ya kisiasa kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kutokana na madai ya baadhi ya viongozi kwamba anatumia handisheki kufaidi ngome yakena kutenga maeneo mengine.

Viongozi kutoka Bonde la Ufa na Magharibi wamemtaja Bw Odinga kama mtu mbinafsi anayetumia ukuruba wake na Rais kufaidi eneo anakotoka licha ya ahadi yake kwamba handisheki inalenga “kufaidi taifa la Kenya kwa ujumla.

”Rais Kenyatta pia ameshutumiwa kwa kumzawidi “ndugu yake kisiasa” kwa miradi ya maendeleo kwa kukubali kumuunga mkono kisiasa na kuzika uhasama wa kisiasa ulioibuliwa na madai ya wizi wa kura za urais katika uchaguzi mkuu uliopita.

Wiki jana, wanasiasa kutoka Bonde la Ufa wakiongozwa na Gavana wa Turkana Josphat Nanok walisema kwamba ingawa hawapingi kuzinduliwa kwa miradi katika eneo la Nyanza, walimtaka Rais kuhakikisha uwepo wa usawa kimaendeleo kote nchini.

“Tunamhimiza Rais kuelekeza jicho lake Rift Valley pia kwa kuhakikisha miradi iliyokwama inafufuliwa,” akasema Bw Nanok katika mkutano wa viongozi wa eneo hilo katika Mkahawa wa Masai Lodge, Kajiado.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na magavana; Stephen Sang (Nandi), Hillary Barchok (Bomet), Jackson Mandago (Uasin Gishu), Stanley Kiptis (Baringo) na zaidi ya wabunge 40.Nao wanasiasa wa Magharibi walimsuta Odinga wakidai ametenga eneo hilo kimaendeleo licha ya kuumuunga mkono katika chaguzi kadha zilizopita.

Wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wabunge Titus Khamala (Lurambi), Christopher Aseka (Khwisero) na Didmus Barasa (Kimilili) walidai kuwa Bw Odinga ametumia handisheki kati yake ya Rais Uhuru Kenyatta kupeleka miradi ya maendeleo eneo la Luo Nyanza pekee na kutelekeza “ngome” yake Magharibi ya nchi.

“Sisi watu wa eneo la Magharibi tunahisi kusalitiwa na Raila. Alikuja kwetu wakati wa chaguzi kuu za 2013 na 2017 tukampa kura nyingi zaidi lakini sasa anatumia handisheki kati yake na Rais Uhuru kupeleka miradi Luo Nyanza,” akasema Bw Malala ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Amani Nationali Congress (ANC).

“Nawaomba watu wetu kumuunga mkono mtoto wetu Wycliffe Musalia Mudavadi katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu Raila ameonyesha wazi kuwa hana moyo wa kushughulikia shida za wakazi wa Magharibi,” akaongeza.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema ni shutuma kama hizi zilizomlazimu Bw Odinga kujitokeza na kuzipuuzilia mbali.Wanasema Odinga aliamua kujitetea kwa hofu kwamba huenda madai hayo yangedidimiza ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka ujao baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

“Japo wanasiasa waliotoa madai hayo si wa hadhi yake kisiasa, Raila aliamua kuwajibu kwa sababu madai yao yana hatari ya kumvua lile joho la kiongozi wa kitaifa na kumsawiri kama kiongozi wa kikabila.

Taswira hii huenda ikamgharimu kisiasa endapo itakolea mawazoni mwa raia,” asema Bw Dismus Mokua.Katika utetezi wake, Bw Odinga alisema kuwa kuzinduliwa kwa miradi hiyo na kuandaliwa kwa sherehe hizo katika eneo la Nyanza hakufai kuchukuliwa kama hatua ya kupendelea eneo hilo, kama baadhi ya wanasiasa walivyodai.

“Naamini kuwa enzi za kuchochea jamii moja dhidi ya nyingine zimeisha. Wale wanaotaka kuwarejesha Wakenya katika enzi hizi wanaishi katika nchi nyingine,” ikasema taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na msemaji wa Odinga Bw Dennis Onyango.

Bw Odinga alisema madai kama hayo yanaenda kinyume na “moyo wa kujenga Kenya yenye umoja na ufanisi kutokana na makabila na maeneo mengi”Alisema viongozi wa kisiasa wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kuendeleza umoja na kuwahimiza wafuasi wao kutumia uwezo na rasilimali walizo nazo kujiendeleza na kustawisha Kenya.

“Sherehe za Madaraka Dei mnamo Juni 1, na shughuli zilizotangulia zinaenda sambamba na mtindo ulioanzishwa mnamo 2013 wa kutoa nafasi kwa kaunti mbalimbali kuonyesha yale ambayo zinaweza kuchangia, kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa, katika ustawi wa Kenya.

”“Hakuna mradi hata mmoja uliozinduliwa kabla ya sherehe za Madaraka Dei unaoendeshwa na kaunti ya Kisumu. Hii ni miradi ya kitaifa ambayo inalenga kufaidi Wakenya wote, husasan wanaotoka ukanda wa Magharibi ya Kenya,” Bw Odinga akafafanua.

Akionekana kuwajibu wanasiasa wa Magharibi, Waziri huyo mkuu wa zamani alieleza kwamba ukarabati wa reli ya zamani kutoka Nakuru hadi Kisumu, utaendelezwa hadi Butere katika kaunti ya Kakamega.“Reli hiyo si ya kipekee inayofanyiwa ukarabati.

Reli nyingine ni ile inayotoka Nakuru kupitia Eldoret na kufika Malaba, mradi ambao utafaidi eneo la Rift Valley,” Bw Odinga akaeleza.Lakini Bw Mokua aliongeza kuwa ni Rais Kenyatta ambaye amesababisha kiongozi huyo wa ODM kujipata katika hali hiyo.

Hii, anasema ni kwa sababu tangu waliporidhiana kisiasa mnamo Machi 9, Rais Kenya hakujitwika wajibu wa kufanya mikutano ya pamoja na Bw Odinga katika sehemu mbalimbali nchini kama njia ya kupalilia umoja wa kitaifa.

“Japo Rais Kenyatta na Raila walisema handisheki ililenga kupalilia umoja wa kitaifa na kwamba wangezunguka kote nchini kuhubiri maridhiano, hilo halikufanyika. Hata kabla ya mlipuko wa Covid-19 mwaka jana, Rais hakuwahi kuandamana na Raila kwenye ziara zake za kuzindua miradi ya maendeleo katika maeneo mengine isipokuwa Nyanza.

Hii imechangia kuwepo kwa dhana kwamba Raila ni kiongozi wa Nyanza pekee,” anasema.Kauli yake, inaungwa mkono na Bw Martin Andati ambaye anasema kuwa licha ya kwamba handisheki ilionekana kama daraja la kumwezesha Bw Odinga kufikia Canaan, sasa imegeuka kuwa jinamizi la kusambaratisha ndoto hiyo.

“Uchaguzi mkuu unapokaribia, mahasidi wa Raila wataendeleza dhana kwamba amenyima maeneo mengine matunda ya handisheki. Itamlazimu kujizatiti kuondoa dhana hiyo uchaguzi mkuu unapokaribia,” anashauri Bw Andati.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wahofia wagonjwa huiba vyandarua vya mbu

Hatukutengewa fedha za referenda, IEBC yafafanua