• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Magavana tumbototo kuhusu miradi waliyoanza

Magavana tumbototo kuhusu miradi waliyoanza

Na SHABAN MAKOKHA

MAGAVANA wanaohudumu katika mihula yao ya mwisho wana wasiwasi kuhusu sifa watakazoacha baada ya miradi mingi waliyoanzisha mara tu baada ya kuchaguliwa kukwama.

Magavana wengi wameendelea kuanzisha miradi mipya katika kaunti zao baada ya ile iliyoanzishwa awali kutomalizika kufikia sasa.Baadhi ya miradi hiyo ilianzishwa tangu 2014 lakini haijamalizika mingi haijakamilika hadi leo.

Wengi wanahofia huenda isiwafae wenyeji kwa namna yoyote ile hata baada ya kutengewa mamilioni ya fedha.Kutokana na hofu hiyo, wengi wanailaumu Wizara ya Fedha kwa kuwa kikwazo kikuu kuhusu ukamilishaji wake, kwa kuchelewesha fedha inazotoa kwa serikali za kaunti.

Baadhi ya miradi hiyo ni shule, barabara, vituo vya afya na maeneo ya michezo. Miradi mingine hata haijawahi kuanza kutekelezwa licha ya kutengewa mamilioni ya pesa.Katika Kaunti ya Kakamega, mzozo umeibuka kati ya Gavana Wycliffe Oparanya na Seneta Cleophas Malala baada ya Bw Malala kumwambia gavana kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa na serikali yake imekamilika kufikia mwaka ujao.

Aliwaomba madiwani katika kaunti kuhakikisha fedha zitakazotolewa kwa kaunti zitatumika kumalizia miradi iliyokwama badala ya mingine kuanzishwa.“Magavana wanaohudumu mihula ya mwisho wanapanga kuanzisha miradi mipya ili kuchukua hongo kutoka kwa wanakandarasi.

Wanataka kuacha miradi hiyo na ile waliyoanzisha kutekelezwa na wale watakaochukua uongozi baada yao kung’atuka. Ninamtaka Bw Oparanya kuhakikisha miradi yote aliyoianzisha imekamilika,” akasema Bw Malala.

Baadhi ya miradi iliyokwama katika kaunti hiyo ni uimarishaji wa Uwanja wa Michezo wa Bukhungu kufikia kiwango cha kimataifa na ukamilishaji wa Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kaunti kwa gharama ya Sh6 bilioni.

Miradi mingine ni Kiwanda cha Majanichai cha Global katika eneo la Shinyalu cha Sh300 milioni. Mradi huo ulizinduliwa mnamo 2017 ijapokuwa hakuna shughuli zozote za ujenzi ambazo zimekuwa zikiendelea tangu wakati huo.

Katika Kaunti ya Busia, kiwanda cha kutengeneza sharubati kilicho katika eneo la Ikapolok, Teso Kaskazini hakijawahi kukamilika. Hii ni licha ya kuzinduliwa miaka sita iliyopita. Kiwanda hicho kilikisiwa kugharimu Sh1.5 milioni.

Kiwanda cha kutengeneza mbolea katika eneo la Korinda na kile cha kutengeneza mihogo katika eneo la Simba Chai, eneobunge la Teso Kusini pia havijaanza kufanya kazi. Ujenzi wa viwanda hivyo ulianza mnamo 2014.

  • Tags

You can share this post!

Mhudumu wa bodaboda anusurika kifo kwa kichapo

Jumba llililoanza kujengwa enzi za Moi latengewa bajeti ya...