• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Amerika kutuma wanajeshi Kenya kupigana na Al-Shabaab

Amerika kutuma wanajeshi Kenya kupigana na Al-Shabaab

BRIAN NGUGI na WALTER MENYA

RAIS wa Amerika Joe Biden ametangaza kuwa atatuma vikosi maalum vya wanajeshi nchini kusaidia juhudi za kupambana na magaidi wa Al-Shabaab.

Haya yamejiri huku watu 13, wakiwemo maafisa wa usalama 10, wakiripotiwa kuuawa mwezi huu, katika mashambulio yanayodaiwa kutekelezwa na magaidi wa Al-Shabaab, sehemu za Kaskazini Mashariki na Pwani.

Kupitia barua kwa Bunge la Congress Amerika ambayo ilifikia Taifa Leo, Rais Biden alisema ameidhinisha kutumwa kwa vikosi maalum nchini Kenya, ambavyo vinatarajiwa kushirikiana na jeshi la Kenya kuangamiza Al-Shabaab.

Idadi ya vikosi vilivyotumwa haikutajwa. Hatua hiyo ya Amerika inatarajiwa kuimarisha usalama katika taifa hili ambalo katika miaka ya hivi majuzi imehangaishwa na mashambulizi ya kinyama ya ufyatuaji risasi na bomu yanayotekelezwa na Al-Shabaab.

Kundi hilo la kigaidi lenye makao yake Somalia linajulikana kuwa na wandani nchini Kenya.Al-Shabaab imekuwa ikishambulia serikali ya Somali na wanajeshi lakini mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ya kikatili katika mataifa jirani, ikiwemo Kenya.

Maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani hasa yamekuwa yakilengwa na magaidi hao lakini hapo mbeleni kumekuwepo na mashambulizi makuu jijini Nairobi, ikiwemo Jumba la Kibiashara la Westgate mnamo 2013 na DusitD2 Complex mnamo 2019.

Al-Shabaab imetangaza wazi nia yake ya kufanya mashambulizi kama njia ya kulipiza kisasi dhidi ya oparesheni ya Kenya ya kukabiliana na shughuli za kigaidi Somalia.Shughuli hizo za Kenya ni sehemu ya Oparesheni ya Umoja wa Mataifa (Amisom) ambayo huenda ikapata nguvu mpya kufuatia tangazo la kuondolewa kwa vikosi vya Amerika kutoka Somalia mwaka jana.

Rais Donald Trump mwaka uliopita aliamrisha kuondolewa kutoka Somalia kwa maafisa wanaokadiriwa kuwa 700 wa Amerika kufikia Januari 15.Pentagon ilisema wakati huo kwamba, wanajeshi hao watatumika katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki – pengine Kenya na Djibouti — na kuendelea kutekeleza uvamizi dhidi ya makundi ya wapiganaji na wanamgambo wa Islamic State ambao ngome zao zimo katika mataifa jirani.

Serikali mpya ya Biden ambayo imesisitiza hadharani kuwa inachukulia Kenya kama mshiriki “mwafaka” katika vita dhidi ya ugaidi, imeanza kubatilisha sera nyingi zilizokuwa zimeanzishwa na Trump.

  • Tags

You can share this post!

Magavana sasa tumbojoto kuhusu miradi iliyokwama

Ubelgiji na Finland wakung’uta Urusi na Denmark...