• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mishi Mboko amshauri Shahbal awe mtiifu kwa ODM

Mishi Mboko amshauri Shahbal awe mtiifu kwa ODM

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Likoni, Bi Mishi Mboko amemshauri mfanyabiashara wa Mombasa, Bw Suleiman Shahbal awe tayari kutii itikadi za chama cha ODM baada ya kutangaza kujiunga nacho wikendi.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bi Mboko alisifu hatua ya Bw Shahbal akisema mtu yeyote yuko huru kujiunga na ODM mradi tu ajitolee kufuata kanuni za chama na awe mwaminifu chamani.

“Chama ni watu kwa hivyo tunamkaribisha mradi tu awe mwaminifu na asimame imara kwa itikadi na manifesto ya chama. Chama chetu ni cha demokrasia na tunapenda kunapokuwa na ushindani maridhawa,” akasema.

Mnamo wikendi, Bw Shahbal alitangaza ameondoka katika Chama cha Jubilee na kujiunga na ODM anapopanga kuwania ugavana 2022.Tikiti ya ODM kuwania ugavana Mombasa inatarajiwa pia kumezewa mate na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Hata hivyo, Bi Mboko ambaye miezi iliyopita alikuwa ameonyesha nia ya kutaka kuwania ugavana katika Uchaguzi Mkuu ujao, alisema atatangaza rasmi kiti atakachowania baadaye “wakati mwafaka utakapofika”.

Gavana Hassan Joho hajatangaza wazi mgombeaji ambaye atamuunga mkono kwa kiti hicho wakati atakapokamilisha hatamu yake ya pili iliyo ya mwisho kikatiba.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Bw Shahbal kuwania ugavana Mombasa kupitia chama tofauti endapo atafanikiwa kupata tikiti ya ODM, baada ya kushindwa alipowania kupitia Wiper 2013 na Jubilee 2017.

You can share this post!

Phil Foden wa Man-City ndiye mwanasoka mwenye thamani ya...

Spurs wamvizia kocha Paulo Fonseca kuwa mrithi wa Jose...