• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Benteke atia saini mkataba mpya wa miaka miwili kambini mwa Crystal Palace

Benteke atia saini mkataba mpya wa miaka miwili kambini mwa Crystal Palace

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI matata raia wa Ubelgiji, Christian Benteke sasa atachezea Crystal Palace hadi mwishoni mwa msimu wa 2022-23 baada ya kutia saini mkataba mpya wa miaka miwili ugani Selhurst Park.

Benteke, 30, alijiunga na Palace almaarufu ‘The Eagles’ mnamo 2016 baada ya kuagana rasmi na Liverpool kwa kima cha Sh3.9 bilioni. Tangu wakati huo, amefungia Palace jumla ya mabao 33 kutokana na mashindano yote.

Baada ya kupachika wavuni jumla ya mabao 15 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Palace, makali ya Benteke yalishuka pakubwa huku akifaulu kutikisa nyavu mara sita pekee kutokana na jumla ya mechi 71 zilizofuatia.

Hata hivyo, alifufua makali yake kwa mara nyingine mnamo 2020-21 na akafungia waajiri wake jumla ya mabao 10 kwenye kampeni za EPL.

“Nina furaha kuendelea kuwa sehemu ya mipango ya baadaye ya Palace. Kikosi kinajivunia wachezaji walio na ari ya kupata mafanikio na benchi ya kiufundi pia imejitolea mno kufaulisha mipango mingi ya kikosi,” akasema Benteke ambaye ni sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na timu ya taifa ya Ubelgiji kwenye fainali zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Kwa mujibu wa Steve Parish ambaye ni mwenyekiti wa Palace, Benteke ni nguzo muhimu katika kikosi chake kinachopania kutoa ushindani mkali zaidi kwenye kampeni za msimu mpya wa 2021-22.

Palace ambao wana wachezaji 15 ambao mikataba yao ugani Selhurst Park inatamatika rasmi kufikia Juni 30, 2021 bado hawajaajiri kocha mpya tangu Hodgson aondoke mwishoni mwa muhula huu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Brazil waanza vyema kampeni za Copa America kwa kucharaza...

Wakazi 3,500 Mwatate hatarini kufurushwa