• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Abdulswamad amcheka Shahbal kwa kuhamahama vyama

Abdulswamad amcheka Shahbal kwa kuhamahama vyama

Na BRIAN OCHARO

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Shariff amepuuzilia mbali hatua ya mfanyabiashara Suleiman Shahbal kujiunga na ODM.

Bw Shahbal wikendi alitangaza amejiunga na ODM kutoka Jubilee anapojiandaa kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao.

Kulingana naye, Bw Shahbal amekuwa akibadilisha chama tangu zamani bila kufanikiwa kushinda ugavana.

“Huwezi kujua, usishangae kama atahamia chama kingine tena kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema mbunge huyo ambaye pia anajiandaa kuwania urithi wa kiti hicho cha Gavana Hassan Joho.

Bw Shahbal aliwania ugavana kupitia Chama cha Wiper mwaka wa 2013 na Jubilee mwaka wa 2017. Kabla uchaguzi wa 2013, alikuwa mwanachama wa ODM lakini wakazozana kisiasa na Bw Joho.

Bw Sharrif alisema kuwa yeye ni mwanachama mwaminifu wa chama cha ODM na hatarajii kukihama kwa ajili ya kujiunga na chama chochote kingine.

“Sijawahi kufikiria na sidhani kama nitawahi kufikiria kubadilisha ushirika wangu wa kisiasa. Nadhani uaminifu ni bei ghali, usiutarajie kutoka kwa watu wenye bei ya kawadia,” alisema.

Kulingana naye, kurudi kwa Bw Shahbal katika chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga haimshtui wala kumtatiza kuhusiana na azma yake ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo.

“Machozi ambayo tumelia pamoja na chama cha ODM na kicheko ambacho pia tumeshirikiana na uongozi wa chama hicho tangu nilipokuwa tu mbunge hadi sasa ambapo ninasimamia kamati ya Uwekezaji wa Umma, yote ni kwa kwa hisani ya ODM,” alisema.

Bw Joho hajatangaza wazi mwanasiasa ambaye angependa arithi ugavana Mombasa kutoka kwake atakapokamilisha hatamu yake ya pili iliyo ya mwisho kikatiba 2022.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa plantains

Spurs waajiri mkurugenzi wa soka kwa mara ya kwanza tangu...