• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Spurs waajiri mkurugenzi wa soka kwa mara ya kwanza tangu 2013

Spurs waajiri mkurugenzi wa soka kwa mara ya kwanza tangu 2013

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamemwajiri Fabio Paratici kuwa mkurugenzi wa soka.

Paratici, 48, aliagana rasmi na Juventus mnamo Juni 3, 2021 baada ya kuwa afisa mkuu wa soka kambini mwa miamba hao wa soka ya Italia kwa kipindi cha miaka 11.

Ni mara ya kwanza tangu 2013 kwa Spurs kumwajiri mkurugenzi wa soka. Paratici kwa sasa anatazamiwa kushirikiana na mwenyekiti Daniel Levy na mkurugenzi wa benchi ya kiufundi, Steve Hitchen, kutafuta kocha atakayerithi mikoba ambayo Jose Mourinho alipokonywa mnamo Aprili 19, 2021.

Baada ya kutibuka kwa mpango wa Spurs kumrejesha Mauricio Pochettino wa Paris Saint-Germain (PSG) au kumwajiri aliyekuwa kocha wa Inter Milan, Antonio Conte, kumekuwepo na tetesi zinazohusisha kikosi hicho na uwezekano wa kushawishi Erik ten Hag wa Ajax, Graham Potter wa Brighton, Brendan Rodgers wa Leicester City, Roberto Martinez wa timu ya taifa ya Ubelgiji na kocha wa zamani wa AS Roma Paulo Fonseca kujiunga nacho.

Hata hivyo, Ten Hag, 51, ametia saini mkataba mpya utakaomdumisha sasa kambini mwa Ajax ya Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) hadi mwisho wa Juni 2023 huku Rodgers akifichua maazimio ya kuendelea kuhudumu ugani King Power baada ya kushindia Leicester Kombe la FA mnamo 2020-21.

Martinez amesisitiza kwamba hana mpango wowote wa kurejelea ukocha katika ngazi ya klabu kwa sasa na kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuongoza Ubelgiji kutwaa taji la Euro mwaka huu. Martinez ambaye ni raia wa Uhispania, aliwahi kudhibiti mikoba ya Everton kwa miaka mitatu kabla ya kupigwa kalamu mnamo 2016.

Ubelgiji ambao wanaorodheshwa na FIFA nambari moja duniani, wataanza kuwinda ufalme wa Euro dhidi ya Urusi mnamo Juni 12. Washindani wao wengine katika Kundi B ni Denmark na Finland.

Chombo cha Spurs kwa sasa kinashikiliwa na kocha Ryan Mason aliyewahi kuwa mchezaji wa kikosi hicho kilichompokeza mikoba ya akademia mnamo 2018.

Ilivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mason, 29, ataendelea kuwa kocha Spurs kwa muda zaidi huku akisaidiana na Chris Powell, Nigel Gibbs, Ledley King, Michel Vorm na Fabio Paritici ambaye sasa ni mkurugenzi wao wa soka. Ni mara ya kwanza tangu 2013 kwa Spurs kuajiri mkurugenzi wa soka kambini mwao.

Conte ambaye amewahi kudhibiti mikoba ya Chelsea, Juventus na Inter Milan, alitarajiwa kutua kambini mwa Spurs baada ya matumaini ya kikosi hicho kumwajiri upya Pochettino kuzaa nunge.

Sasa majadiliano kati ya Conte na vinara wa Spurs yametamatika ghafla huku ikiarifiwa kwamba hakuna uwezekano wowote kwa mazungumzo hayo kurejelewa.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror nchini Uingereza, Conte alikuwa na shaka kuhusu kiwango cha bajeti ambayo Spurs wangempa kwa ajili ya kusajili wanasoka wapya katika soko la uhamisho muhula huu.

Huku Conte akifahamika pakubwa kwa mazoea ya kujinyakulia wanasoka wazoefu sokoni, Spurs wamekuwa wakiongozwa na falsafa ya kuwakuza wachezaji chipukizi na kuwatumia kukisuka kikosi chenye uwezo wa kutoa ushindani mkali katika soka ya Uingereza na bara Ulaya. Hilo ni jambo ambalo Pochettino alifaulu kulifanya kambini mwa kikosi hicho kilichomtimua mnamo 2019.

Kutofaulu kwa mpango wa Spurs kumwajiri Conte kunasaza kikosi hicho katika kibarua cha kuendelea kusaka kocha mpya, wiki 10 tangu Mourinho apate hifadhi mpya kambini mwa AS Roma nchini Italia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Abdulswamad amcheka Shahbal kwa kuhamahama vyama

Mfanyabiashara Chris Kirubi afariki akiwa na umri wa miaka...