Chama cha wazazi chataka serikali iwaandame walimu wakuu watozao ada za haramu

Na TITUS OMINDE

MWENYEKITI wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) Nicholas Maiyo ameitaka Wizara ya Elimu kuwachukulia hatua baadhi ya walimu wakuu wa shule za upili ambao wanaendelea kuwatoza wazazi ada zisizo halali.

Akiongea na wanahabari mjini Eldoret Bw Maiyo alisema hatua hiyo ni kinyume cha mwongozo wa karo ambao ulitolewa na serikali kuu.

Alimtaka Waziri wa Elimu Prof George Magoha kuchukua hatua ya haraka na kuwachunguza walimu wakuu ambao wanatoza ada za ziada ili kuwaondolea wazazi mzigo wakati kama huu ambapo wengi wao wameathirika na janga la corona.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya walimu wakuu wanatumia agizo la waziri Magoha kwamba wazazi wakamilishe karo kwa kuwafukuza hata wanafunzi ambao hawajalipiwe ada zisizoorodheshwa kwenye mwongozo wa karo,” akasema Bw Maiyo.

Wiki jana, Waziri huyo wa Elimu aliwataka wazazi kuhakikisha wamelipa karo yote ya muhula wa tatu.

Alisema kuna baadhi ya wazazi wenye uwezo kifedha ambao wanakataa kulipa karo kimakusudi na hivyo kuziweka shule husika katika matatizo ya kifedha.

“Nawaamuru walimu wakuu kuwatuma nyumbani wanafunzi ambao wazazi wao hawajakamilisha kulipa karo ilhali kuna ushahidi kwamba wana uwezo wa kufanya. Hata hivyo, wanafunzi kutoka familia masikini wasifukuzwe bali wazazi wao wazungumze na walimu ili waelewane kuhusu utaratibu wa kulipa karo,” akasema Bw Magoha.

Hata hivyo, Bw Maiyo anasema ana ushahidi wa kuonyesha kuwa kuna walimu wakuu wanaotoza wazazi kima cha Sh6,000 kama ada zisizo halali.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

Habari zinazohusiana na hii

Hakuna kupumua shuleni

Waziri mtatanishi