• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
Sheria za mashabiki kujiweka salama Safari Rally zatangazwa

Sheria za mashabiki kujiweka salama Safari Rally zatangazwa

Na GEOFFREY ANENE

WAANDALIZI wa Mbio za Magari za Dunia (WRC) za Safari Rally wametangaza sheria za usalama zinazofaa kuzingatiwa na mashabiki wasipatwe na balaa.

Maelfu ya mashabiki wanatarajiwa kujitokeza katika barabara za mashindano kutazama madereva wakipaisha magari yao katika duru hiyo ya dunia mnamo Juni 23-27.

Waandalizi wamesema kuwa mashindano mazuri ni yale ambayo ni salama.

“Usalama ni muhimu kabisa katika Safari Rally 2021. Mashabiki wanafaa kufahamu sheria za kiusalama na kuhakikisha wanajiweka salama wakati wa mashindano hayo ya kihistoria,” Shirikisho la Mbio za Magari Kenya (KMSF) lilitangaza hapo Juni 14.

Katika sheria hizo, mashabiki wameonywa dhidi ya kusimama barabarani, kusimama katika maeneo yaliyopigwa marufuku, kusimama ama kuketi karibu na ua ama ukuta kando ya barabara, kukaa karibu sana na barabara na kuzuia njia za kutorokea.

Mashabiki pia wanahitajika kuwa macho wakati wote na wasithubutu kuondoa alama za barabara za mashindano.

Isitoshe, mashabiki wameonywa kuwa watarajie chochote, wasikize kwa makini gari linalokaribia, wawe macho kabisa, wahakikishe wako na nafasi ya kuhepa wanapohitajika kufanya hivyo na wajaribu kusimama nyuma ya kitu ambacho kiko imara.

Watoto wanafaa kuwa chini ya uangalizi. Mashabiki pia wanafaa kufuata maagizo ya waelekezaji barabarani na pia kuwasaidia kuhakikisha mashindano ni salama.

Mashabiki wamekatazwa kabisa kusimama kwenye kona na makutano ya barabara.

“Unaonywa kuwa mbio za magari zinaweza kuwa hatari kwa hivyo jilinde na linda wale wako karibu nawe,” sheria hizo zinasema.

You can share this post!

Chama cha wazazi chataka serikali iwaandame walimu wakuu...

Uhispania na Uswidi waumiza nyasi bure kwenye kipute cha...