• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Shule mpya ya msingi ya Mutuya yafunguliwa Ruiru

Shule mpya ya msingi ya Mutuya yafunguliwa Ruiru

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE mpya ya msingi ya Mutuya imefunguliwa eneobunge la Ruiru ili kupunguza msongamano uliopo katika shule ya Mwihoko iliyoko Githurai.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara amesema serikali kuu imefanya juhudi kuona ya kwamba shule hiyo inajengwa ili kupunguza msongamano mkubwa ambao umekuwa katika shule ya Mwihoko.

“Kwa muda mrefu shule ya Mwihoko imekuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi huku ikikumbatia wanafunzi wapatao 4,000. Hata walimu wamekuwa na wakati mgumu wa kufundisha kwa wanafunzi katika madarasa hayo,” alisema Bw King’ara.

Alipozuru shule hiyo mpya ya Mutuya mnamo Jumanne, amejionea wanafunzi 1,500 waliopelekwa huko kutoka Mwihoko.

Ameeleza kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa sababu wanafunzi watapata afueni ya kusomea katika mazingira yafaayo.

Mnamo mwezi Januari 2021 Waziri wa Elimu Prof George Magoha alizuru shule hiyo na kukiri kuwa kulikuwa na haja ya kujengwa madarasa mapya eneo lingine ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wengine kupelekwa huko.

Alisema kutokana na hali ilivyo ya janga la Covid-19, ni vyema wanafunzi kupunguzwa na kupelekwa kwingineko.

Mbunge huyo amesema tayari kuna mipango ya kuongeza madarasa mengine katika eneo la Kiu, na Mwalimu Farm, eneo la Kwihota mjini Ruiru.

Alieleza pia ameendesha miradi kadha katika shule kadha kwa kutumia hazina ya ustawishaji maeneobunge NG-CDF.

Alitaja Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ruiru kama mojawapo ya shule ambazo zimenufaika na mgao wa NG-CDF.

Alieleza kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu 2021 kutakuwa na mabadiliko makubwa ambapo Shule ya Msingi ya Mwihoko itapata afueni ya kuwa na wanafunzi wanaohitajika bila kuwa na msongamano.

Bw Peter Mwangi ambaye ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma kwenye shule ya Mwihoko alisema hatua iliyochukuliwa na serikali ni ya kupongezwa kwa sababu msongamano utaisha.

“Watoto wetu wamekuwa wakisomea katika mazingira magumu ajabu madarasani, lakini sasa mambo yatabadilika na kuwa afadhali,” alisema Bw Mwangi.

Naye Bi Mary Muthoni ambaye pia ni mzazi alisema watoto wengi wanaoishi karibu na shule mpya watapata wakati mzuri kwani hawatatembea mwendo mrefu kufika shuleni.

You can share this post!

Njia asili ya kuondoa visunzua yaani warts

Serikali yasaidia wanavoliboli ya ufukweni Kenya kuwania...