• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Serikali yasaidia wanavoliboli ya ufukweni Kenya kuwania tiketi ya Olimpiki nchini Morocco

Serikali yasaidia wanavoliboli ya ufukweni Kenya kuwania tiketi ya Olimpiki nchini Morocco

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya voliboli ya ufukweni itaondoka nchini Ijumaa kuelekea Morocco kushiriki mashindano ya kupigania tiketi ya kuingia Olimpiki yatakayoandaliwa mjini Agadir mnamo Juni 19-29.

Kocha Sammy Mulinge alieleza Taifa Leo hapo Jumanne kuwa kulikuwa na wasiwasi kuhusu safari ya timu ya Kenya.

“Hatukujua kama tunasafiri ama la, lakini tumepata usaidizi kutoka kwa serikali na sasa tutaondoka Ijumaa,” alisema Mulinge.

Kenya itawakilishwa na timu nne katika mashindano hayo maarufu kama Continental Cup, yatakayoanzia raundi ya pili.

Katika kitengo cha kinadada, Kenya itawakilishwa na Brackcides Agala akishirikiana na Gaudencia Makokha, na Yvonne Wavinya na Phosca Kasisi. Wanaume ni Ibrahim Oduor/James Mwaniki na Brian Melly/Enock Mogeni.

Wilfred Kimutai, Cornelius Lagat, Donald Mchete, Evans Bera, Maureen Nekesa, Veronica Adhiambo na Naomi Too hawakufaulu kuingia kikosi kitakachosafiri.

Timu ya Kenya imekuwa ikifanyia mazoezi yake katika ufuo wa hoteli ya Flamingo Beach Resort mjini Mombasa. “Tumekuwa hapa kwa majuma mawili. Hatukuweza kufanya mazoezi kwa muda mrefu kutokana na masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Hata hivyo, tuko tayari. Motisha ya timu iko juu,” aliongeza Mulinge.

Kocha huyo alionyesha kuridhika kuwa wachezaji wake wameimarika. “Uchezaji wao wa voliboli ya ufukweni umeimarika. Walikuwa wamezoea voliboli ya kawaida. Wanasogeza miguu yao kwenye changarawe kwa haraka kuliko walipokuwa wakianza voliboli ya ufukweni. Pia, wamepata kufahamu vitu kadhaa muhimu vya mchezo huu. Kwa mfano, hakuna kubadilisha wachezaji hadi mechi itamatike. Hii inahitaji kufundishwa kuwa lazima wachezaji wawili walio uwanjani wajiweke vyema kisaikolojia.”

Timu 17 za kitaifa za kinadada na 24 za wanaume zinatarajiwa kuhudhuria mashindano hayo mjini Agadir.

  • Tags

You can share this post!

Shule mpya ya msingi ya Mutuya yafunguliwa Ruiru

Ashley Young akataa ofa ya kusalia Inter Milan na anatamani...