• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Ureno waanza kutetea taji la Euro kwa kuadhibu Hungary na kutua kileleni mwa Kundi F

Ureno waanza kutetea taji la Euro kwa kuadhibu Hungary na kutua kileleni mwa Kundi F

Na MASHIRIKA

TIMU ya taifa ya Ureno ilianza vizuri vita vya kutetea ubingwa wa Euro kwa kuwapokeza Hungary kichapo cha mabao 3-0 kwenye mchuano wa kwanza wa Kundi F mnamo Jumanne.

Mechi hiyo ilisakatiwa mbele ya mashabiki 60,000 katika uwanja wa Puskas Arena jijini Budapest.

Kiungo Raphael Guerreiro aliwaweka Ureno kifua mbele katika dakika ya 84 kabla ya nyota Cristiano Ronaldo kufunga mabao mawili ya katika dakika za 87 na 90 mtawalia.

Tangu waambulie nafasi ya tatu kwenye Euro mnamo 1964 na kukamata nambari ya nne mnamo 1972, Hungary hawakuwahi kufuzu kwa fainali za kipute hicho hadi 2016.

Ingawa walijibwaga ulingoni wakijivunia rekodi ya kutopoteza mechi yoyote kati ya 11 za awali, Hungary walizidiwa ujanja na masogora wa Ureno wanaonolewa na kocha Fernando Santos.

Dalili zote ziliashiria kwamba mechi hiyo ingekamilika kwa sare tasa hadi Hungary walipoishiwa pumzi katika dakika sita za mwisho na kuruhusu Ureno kuwafunga mabao matatu ya haraka.

Bao la Guerreiro lilitokana na tukio la beki Orban wa Hungary kubabatizwa na mpira baada ya presha tele kutoka kwa mafowadi wa Ureno waliotegemea pakubwa huduma za Ronaldo, Bernardo Silva wa Mancheter City, Diogo Jota wa Liverpool, Joao Felix wa Atletico Madrid na Bruno Fernandes wa Manchester United.

Ureno walijibwaga ugani kupepetana na Hungary wakijivunia huduma za wanasoka saba wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika kikosi chao cha 11-bora. Hao walikuwa Jota, Joao Moutinho wa Wolves, Fernandes, kipa Rui Patricio wa Wolves, beki Nelson Semedo wa Wolves, Silva na difenda Ruben Dias wa Man-City.

Hungary kwa sasa wanajiandaa kwa mchuano wao wa pili kundini dhidi ya Ufaransa mnamo Juni 19 jijini Budapest huku Ureno wakipepetana na Ujerumani jijini Munich.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ufaransa wang’aria Ujerumani kwenye gozi kali la Euro

AKILIMALI: Ufugaji wa samaki bila gharama kubwa