• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
AKILIMALI: Ufugaji wa samaki bila gharama kubwa

AKILIMALI: Ufugaji wa samaki bila gharama kubwa

Na SAMMY WAWERU

SAMAKI ni kati ya wanyama wa majini wanaoweza kufugwa nyumbani na ambao ufugaji wake haujakumbatiwa na wengi.

Idadi ya wanaofuga samaki nchini ni ya chini mno, suala ambalo linachangia bei ya wanyama hawa kuwa ghali.

Licha ya upungufu huo, wameibuka kuwa kipenzi cha wengi, kutokana na manufaa yake kiafya.

Aidha, samaki ni miongoni mwa nyama nyeupe, ambayo ina kiwango cha juu cha Omega 3, madini muhimu katika mwili wa binadamu.

Isitoshe, ni chanzo bora cha madini ya Protini.

Huku wanyama hao wakiwa na ushindani mkuu sokoni, kwa wenye vipande vya ardhi na chanzo cha maji safi ni rahisi kuingilia ufugaji wake.

Patrick Kamau ni mfugaji wa samaki eneo la mjini, na anasema muhimu ni kuwa na ufahamu pekee.

Kulingana na mfugaji huyu wa aina yake Nairobi, samaki ni kati ya wanyama rahisi kufuga.

“Wanachohitaji ni kidimbwi au vidimbwi na chanzo cha maji safi na ya kutosha,” Kamau anasema.

Anaongeza: “Ikija upande wa lishe, hawali chakula kingi. Wanapewa chakula kwa kipimo.”

Mosi, ni kuanza na utafiti, unaojumuisha kujua soko tayari, jinsi ya kuwafuga na kuwatunza.

Paul Nyota ni mfugaji chipukizi wa wanyama hawa, eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Kwa sasa ana dimbwi moja, aliloandaa kwa kulichimba kwa mikono.

“Baada ya kulichimba, kandokando (kutani) na chini (sakafu) weka karatasi ngumu ya nailoni au plastiki, maarufu kama dam liner,” Nyota anaelezea.

 

Paul Nyota, mfugaji chipukizi wa samaki eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Wakati wa maandalizi, unahimizwa kuhakikisha umetengeneza mkondo au mwanya wa kuondoa maji.

Samaki hulishwa chakula maalum aina ya pellets na pia majani ya mboga.

Kuna chakula kingine, na ambacho wafugaji wanashauriwa kukikumbatia, wadudu aina ya Funza Kibaha.

Wadudu hao maarufu kama Black Soldier Flies (BSF), wataalamu wanawasifia kusheheni virutubisho vya Protini, madini muhimu mno kwa samaki na kuku.

“Samaki wanahitaji Protini kwa wingi ili kukua haraka. BSF wana kiwango cha juu cha Protini,” anaelezea Francis Faluma, mtaalamu na afisa wa masuala ya samaki kutoka Serikali ya Kaunti ya Kakamega.

Kwa mujibu wa maelezo ya Faluma, BSF ni chanzo bora cha Protini, wakilinganishwa na vyakula kama maharagwe ya soya, chakula cha madukani, mbegu za pamba, kati ya vinginevyo.

Dimbwi lenye ukubwa wa mita 17 kwa 7, lina uwezo kusitiri kati ya samaki 2,000 hadi 3,000.

Katika masoko mengi ya bei jumla, samaki mmoja hapungui Sh100.

Samaki wanaoshabikiwa na wengi ni Tilapia na kambare (catfish).

Ufugaji wa kisasa, wa matumizi ya dam liners, si kama ule wa zamani kuchimba mabwawa au vidimbwi na kukorogea saruji, na ambao ni ghali.

Kando na kuandaa vidimbwi kwa njia ya kuchimba, unaweza kuvitengeneza kwa kutumia mbao, viwe na umbo la mstatili, kisha kandokando na chini utumie dam liners.

Juu, weka neti ili kuzuia nyuni wa kawaida na pia mwewe dhidi ya kuwashambulia.

You can share this post!

Ureno waanza kutetea taji la Euro kwa kuadhibu Hungary na...

Magari matatu ya Sh13 milioni kila moja kutumiwa na...