• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Wanaokabiliwa na njaa wasajiliwa ili wasaidiwe

Wanaokabiliwa na njaa wasajiliwa ili wasaidiwe

KNA na MAUREEN ONGALA

Mamlaka ya Taifa ya kukabiliana na Ukame (NDMA), jana ilianza kuwasajili watu wanaokabiliwa na njaa Kaunti ya Tana River, ili wanufaike na Mpango wa Kinga dhidi ya njaa (HSNP).

Mpango huo unalenga familia 7, 377 katika kaunti hiyo ambazo zitapokea Sh2700 kila mwezi huku Sh239 milioni zikitumiwa kwa mpango huo kwa mwaka.

Gavana wa Tana River Dhadho Godhana aliyezindua zoezi hilo katika Gururi, eneobunge la Galole alihimiza watakaonufaika kutumia vizuri pesa hizo na kuwekeza sehemu yake kwa shughuli za kuwaletea mapato.

“Nina imani na matumaini kwamba kutumiwa pesa kutachangia pakubwa katika kuimarisha maisha ya kifedha ya familia maskini na kaunti kwa jumla. Kwa kuwa watu wetu kwa kawaida wana bidii, niko na imani kwamba familia hizi zitawezekeza baadhi ya pesa,” alisema Gavana Godhana.

Alisema kwamba usajili huo utasaidia kupata habari ambazo zitatumiwa kutoa misaada ya kibinadamu majanga yakitokea.

“Tukiwa na habari hizi katika sajili yetu ya kijamii, serikali yangu itanufaika kwa kuwa itazitumia kulenga jamii ambazo hazijakuwa zikifikiwa na mashirika mengine ya kutoa misaada ya binadamu wakati wa ukame na mafuriko,” alisema.

Kulingana na mshirikishi wa NDMA katika kaunti hii Bw Abdi Musa, usajili huo na familia kutumiwa pesa kutafanywa kutoka nyumba hadi nyumba kwa kutumia mfumo wa kubaini eneo wa GPS.

Alisema atahakikisha kwamba kila eneo litakuwa na watu watakaonufaika kwa mpango huo ili pesa zifike sehemu zote za kaunti hiyo. Mpango wa HSNP pia umetekelezwa kaunti za Turkana, Wajir, Mandera na Marsabit ambako familia 101,800 hutumiwa pesa za kujikimu na serikali. Serikali inapanua mpango huo hadi kaunti za Tana River, Isiolo na Samburu ili kukinga familia maskini katika maeneo kame ambako familia 3,200 zitanufaika katika awamu ya kwanza katika kaunti hizi.

Gavana Dhadho alisema serikali yake imejitolea kupunguza njaa kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo. “Serikali yangu imesaidia wakulima katika kaunti na mimea inayostahimili ukame hasa katika maeneo ya Bura na Upper Hola ili kuhakikisha kuna chakula cha kutosha kauntini,” alisema.

Serikali ya kitaifa ina mipango mingine ya kukinga watoto mayatima na walio kwenye hatari (OVC), watu walio na ulemavu (PWSD) na wazee. Katika kaunti ya Kilifi, wabunge wametoa wito kwa serikali kuu itenge pesa za kutosha kuepusha maafa yanayoweza kusababishwa na njaa.

Hii ni baada ya wizara inayosimamia masuala ya majanga katika kaunti hiyo kusema huenda watu milioni 1.2 wakataabika kwa njaa na kiu kuanzia hivi karibuni. Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya alisema atawasilisha hoja bungeni ili serikali kuu itenge pesa za kutosha kutoa misaada kwa wale wanaotarajiwa kuathiriwa na athari za kiangazi.

“Tunaelekea katika hali mbaya ya ukame na watoto wetu watapata shida wakati ambapo watahitajika kuwa shuleni,” akasema.

You can share this post!

Uzinduzi wa chama kipya Mlima Kenya waahirishwa

Majonzi Afrika baada ya shujaa wa ukombozi Kenneth Kaunda...