Kemri kubaini athari ya chanjo kwa Wakenya

Na MAUREEN ONGALA

TAASISI ya Utafiti wa Matibabu nchini Kenya (Kemri) inatarajia kukamilisha utafiti wake kuhusu ikiwa chanjo ya Astrazeneca ina athari hasi kwa Wakenya kufikia mwishoni mwa mwezi ujao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kemri, Prof Samuel Kariuki alisema chanjo hiyo inayofahamika kisayansi kama ChAdOx1n CoV-19 inaendelea kutumiwa nchini kwa sababu kuna hali ya dharura, lakini uchunguzi kuhusu athari zake kwa Wakenya ulikuwa bado unaendelea.

Akizungumza wakati kamati ya bunge kuhusu afya ilitembelea shirika hilo katika Kaunti ya Kilifi, Prof Kariuki alisema baadhi ya mataifa yalikuwa yamekamilisha utafiti kuhusu athari za chanjo hiyo kwa raia wao kwa sababu walianza mapema.

“Kulikuwa na janga na ilionekana kuwa chanjo zilikuwa zinafaa, kwa hivyo ilikuwa bora kuzitumia kuliko kukaa bure. Tutakamilisha majaribio yetu kwa chanjo hiyo kufikia mwisho wa Julai,” akasema.

Wakati utafiti wa kubainisha athari za chanjo hiyo kwa Wakenya ulipoanzishwa Kilifi mwaka uliopita, KEMRI ilisema hatua hiyo huwa ni muhimu kwa sababu chanjo yoyote ile huwa inaweza kuwa bora kwa watu wa sehemu moja ya ulimwengu lakini iwe na athari tofauti kwa watu wanaotoka sehemu nyinginezo.

Kwa mujibu wa KEMRI, hali kama hii imewahi kushuhudiwa katika chanjo za magonjwa mengine kama vile malaria na Ebola.

Wakenya kadhaa walikuwa wamejitolea kufanyiwa majaribio ya chanjo hiyo ya ChAdOx1n CoV-19 miilini mwao ndipo ibainike ikiwa kuna matokeo yoyote ya kipekee yanayofaa kuzingatiwa na wananchi.

“Huwa ni muhimu kufanya utafiti wa aina hii kwa wananchi wetu kwa sababu kinga za magonjwa miilini mwa binadamu hutofautiana kama vile kwa msingi wa tofauti za hali ya hewa,” akaeleza Prof Kariuki.

Kamati ya bunge inayosimamia masuala ya afya ilitoa wito kwa serikali iongeze mgao wa fedha unaotumiwa kwa utafiti katika shirika hilo ili lifanikishe mipango yake kwa manufaa ya wananchi.

Wabunge

Wakiongozwa na Mbunge wa Ndhiwa, Bw Martin Owino, wabunge hao walisema nchi hii itaendelea kuwa hatarini kukumbwa na majanga ya magonjwa ikiwa KEMRI haitafadhiliwa vyema kuendesha utafiti wa matibabu.

“Hakuwezi kuwa na maendeleo katika nchi ambapo wananchi ni wagonjwa. Tuna taasisi iliyo na uwezo mkubwa lakini hatuitumii kikamilifu. Tunataka ufadhili uongezwe ili watafiti wawe katika kiwango sawa na taasisi nyingine za utafiti wa matibabu ulimwenguni,” akasema.

Msimamo sawa na huu ulitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kemri, Dkt Daniel Mbinda ambaye alisema utafiti katika afya ni msingi bora unaoweza kustawisha sekta nyingine zinazotegemewa kwa uchumi wa taifa.

Habari zinazohusiana na hii