• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
AFYA: Je, virusi vya HIV vinachochea corona?

AFYA: Je, virusi vya HIV vinachochea corona?

TANGU takwimu za wizara ya Afya zilipoanza kuonyesha kuwa maambukizi ya virusi vya corona yameongezeka katika ukanda wa Ziwa Victoria, kumekuwa na madai tele katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao wamekuwa wakidai kuwa idadi kubwa ya vifo vinavyohusiana na corona huenda ikashuhudiwa katika eneo la Ziwa Victoria ambalo linaongoza kwa visa vingi vya maambukizi ya HIV.

Aidha ripoti iliyochapishwa wiki iliyopita na mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa kuhusu mwanamke anayeishi na virusi vya HIV na ambaye alikuwa na virusi vya corona mwilini kwa miezi saba (siku 216) nchini Afrika Kusini, imezidisha hofu miongoni mwa Wakenya mitandaoni.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 36, aliambukizwa virusi vya HIV mnamo 2016 na kingamwili (immunity) yake ilikuwa imefifia licha ya kutumia dawa za kupunguza makali-ARVs.

Kulingana na mtandao wa Business Insider, inadaiwa kuwa mwanamke huyo aliambukizwa virusi vya corona mnamo Septemba 2020 na akapona baada ya miezi saba baada ya virusi hivi kujibadilisha mara 30. Aidha alipatikana na aina mbalimbali za corona.

Serikali, wiki iliyopita iliweka vikwazo zaidi katika juhudi za kudhibiti maambukizi katika Kaunti za Busia, Vihiga, Kisii, Nyamira, Kakamega, Kericho, Bomet, Bungoma, Trans-Nzoia, Kisumu, Siaya, Homa-Bay na Migori.

Wizara ya Afya ilifunga maeneo ya kuabudu, ilipiga marufuku mikutano na kuongeza muda wa kafyu na sasa wakazi hawataruhusiwa kuwa nje kati ya saa 1.00 jioni hadi saa 10.00 alfajiri.Kulingana na wizara ya Afya, Kaunti hizo 13 sasa zinachangia asilimia 60 ya maambukizi mapya ya virusi vya corona nchini.

Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na Magavana wa Kaunti za Ukanda wa Ziwa (LREB) wanaoongozwa na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, ilionyesha kuwa kaunti hizo zimelemewa na makali ya corona na sasa zinahitaji kwa dharura vifaa vya kukinga wahudumu wa afya (PPEs), wahudumu zaidi wa afya, mashine za kupima virusi, vitanda, mitungi ya oksijeni, vyumba zaidi vya wagonjwa mahututi (ICU) na mifuko ya kuweka maiti.

Isaiah Odundo ambaye ni mkazi wa eneo la Kisian, katika Barabara ya Kisumu-Busia, anasema kuwa idadi ya matanga imeongezeka katika eneo hilo – hali inayomfanya kuamini kuwa maradhi ya corona ndio yanaua watu kwa kasi.

“Tusidanganyane, ugonjwa wa corona upo na unaua watu wengi. Karibu katika kila boma kumetokea matanga hivi karibuni,” anasema Bw Odundo.

Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma, anasema kuwa hospitali zimejaa kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa corona katika Kaunti hiyo.

“Vyumba vya ICU vimejaa. Idadi kubwa ya watu wanafariki kutokana na corona katika eneo-bunge langu. Wiki iliyopita nilipoteza mama mkwe wangu baada ya kuugua corona kwa siku nane na tulilipa Sh2.3 milioni,” anasema Bw Kaluma.

Hali hiyo ndiyo imesababisha baadhi ya Wakenya kuhofia kuwa huenda virusi vya HIV vinachangia kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona na vifo katika kaunti za ukanda wa Ziwa Victoria.

Ripoti ya hivi karibuni ya wizara ya Afya inaonyesha kuwa kasi ya maambukizi ya virusi vya HIV katika Kaunti za Homa Bay, Kisumu, Siaya, Migori, Kisii, Vihiga na Busia iko juu ya wastani wa kitaifa.Wastani wa kitaifa wa maambukizi ya HIV nchini ni asilimia 4.6. Maeneo ya vijijini yanaongoza kwa maambukizi ya HIV kuliko maeneo ya mijini.

Jumla ya watu milioni 1.6 wanakadiriwa kuishi na virusi vya HIV. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa idadi ya watu wanaofariki kila mwaka nchini kutokana na ugonjwa wa Ukimwi imepungua ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.Kasi ya maambukizi ya HIV katika Kaunti ya Homa Bay ni asilimia 19.6, Kisumu (asilimia 17.5), Siaya (asilimia 15.3), Migori (asilimia 13.9), Busia (asilimia 9.9), Kisii (asilimia 6.19) na Vihiga (asilimia 5.3).Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman, anasema kuwa asilimia 90 ya watu wanaoishi na HIV wanatumia dawa za kupunguza makali (ARVs).

“Asilimia 90 ya wanaotumia ARVs wamepunguza makali ya virusi vya HIV kiasi kwamba ni vigumu kuambukiza wengine,” anasema Dkt Aman.

Je, virusi vya HIV vinaweza kusababisha waathiriwa kulemewa na ugonjwa wa corona?

Dkt Aman anasema kuwa ni idadi ndogo sana ya watu wanaoishi na virusi vya HIV wanaolemewa na ugonjwa wa corona.

“Hii ni kwa sababu wengi wa waathiriwa wa HIV wanatumia tembe za ARVs hivyo kingamwili zao ni imara,” anasema Dkt Aman.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Nairobi, Wizara ya Afya pamoja na taasisi nyinginezo za kimataifa, ulionyesha kuwa idadi kubwa ya watu wanaolemewa na virusi vya corona wanaugua maradhi ya moyo na kisukari.

Miongoni mwa watu waliolazwa hospitalini baada ya kupatwa na virusi vya corona kati ya Aprili na Novemba mwaka jana, asilimia 17 walikuwa na maradhi ya moyo, kisukari (15), HIV (asilimia 7), Kansa (asilimia 4), matatizo ya figo (asilimia 3) kati ya mengineyo.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa mtu mmoja kati ya watano wanaofariki, ana maradhi ya kisukari.

Wazee wa kuanzia miaka 60 walio na ugonjwa wa kisukari wako katika hatari kubwa zaidi ya kufariki kutokana na corona ikilinganishwa na vijana, kwa mujibu wa WHO.Inakadiriwa kuwa watu 500,000 wana ugonjwa wa kisukari nchini Kenya.

Shirika la WHO linaonya kuwa waathiriwa wa HIV ambao hawatumii ARVs wanaweza kuwa katika hatari ya kulemewa na corona kwani kingamwili zao huwa dhaifu.Kituo cha Kudhibiti Maradhi (CDC) kinasema kuwa hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa watu wanaoishi na virusi vya HIV wako katika hatari ya kuambukizwa au kulemewa na virusi vya corona.

“Tafiti zilizofanywa na Ulaya na Amerika, zilionyesha kuwa hakuna tofauti ya maambukizi baina ya watu wanaoishi na HIV na wenzao ambao hawana,” inasema CDC kupitia tovuti yake.

“Kwa mfano, katika moja ya tafiti zilizofanywa, watafiti walihusisha wanaume 253 waliokuwa na virusi vya HIV na corona na wengine 504 ambao walikuwa na corona bila virusi vya HIV. Walibaini kuwa hakukuwa na tofauti ya vifo au kulazwa ICU kati ya makundi hayo mawili,” inaongezea.

CDC inasema kuwa waathiriwa wa HIV ambao kingamwili zao ni dhaifu ndio wako katika hatari zaidi ya kulemewa na corona.

“Watu wanaofaa kupewa uangalizi wa karibu ni wazee wa zaidi ya miaka 60; wanawake wajawazito; na waathiriwa wa magonjwa kama vile shinikizo la damu, selimundu (sickle cell); wanene kupindukia na watu waliobadilishiwa viungo kama vile figo.

“Hata hivyo, waathiriwa wa HIV walio na magonjwa mengine kama vile shinikizo la damu wako katika hatari zaidi ya kulemewa na virusi vya corona,” kinasema kituo cha CDC.

You can share this post!

Serikali yanyenyekea kuhusu amri kwa makanisa

CECIL ODONGO: Tumjuavyo huyu Kalonzo, atakunja mkia tu