• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Chama chake Abbiy kifua mbele uchaguzini Ethiopia

Chama chake Abbiy kifua mbele uchaguzini Ethiopia

Na MASHIRIKA

CHAMA cha Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kinatarajiwa kunyakua viti vingi vya ubunge katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana.

Chama tawala cha Prosperity Party chake Abiy, kilisimamisha idadi kubwa ya wawaniaji wanaotaka kuwa wabunge wa bunge la kitaifa.

Baadhi ya vyama vya kisiasa vilisusia uchaguzi wa jana hivyo kufanya baadhi ya wawaniaji wa chama tawala kukosa upinzani mkali.

Miongoni mwa vyama vilivyosusia ni Oromo Liberation Front (OLF), ambacho kinalalamikia kufungwa baadhi ya viongozi wake.

Chama cha OLF kina uungwaji mkubwa katika jimbo la Oromia.Raia wa Ethiopia jana walichagua wabunge wa bunge la kitaifa na wabunge wa mabunge ya majimbo.

Waziri mkuu atachaguliwa na wabunge wa kitaifa na kuunda serikali ijayo.Kwa kawaida chama kilicho na wabunge wengi ndicho hutoa waziri mkuu.Abiy 44, alichaguliwa kwa mara ya kwanza 2018 kuongoza taifa hilo lililo na watu milioni 110.

Wapigakura milioni 38 walijisajili kushiriki katika kuchagua wabunge katika maeneobunge yote 547.Shughuli ya kupiga kura jana ilitatizika katika baadhi ya maeneo kutokana na ukosefu wa usalama na kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura.

Maeneo ambayo hayakupata fursa ya kushiriki uchaguzi wa jana yatapiga kura Septemba 6, mwaka huu.Uchaguzi huo haukufanyika katika jimbo la Tigray ambalo linakabiliwa na mapigano.

Tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi jimboni Tigray lililo na viti 38 vya ubunge katika bunge la taifa, haijawekwa.Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa watu 350,000 wanakabiliwa na njaa jimboni Tigray.

Wagombeaji 9,500 walishiriki katika uchaguzi huo kwenye ngazi za kitaifa na majimbo.Kamati ya uchaguzi imesema kuwa uchaguzi wa jana utakuwa huru na haki.

Waziri mkuu Ahmed alimteua Birtun Mideska, aliyekuwa jaji wa ngazi ya juu hapo awali, kuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi.

Mideska ambaye ni kiongozi wa upinzani alikuwa akiishi uhamishoni kabla ya kurejea nchini Ethiopia.

Waangalizi wa kimataifa na nchini humo walishiriki katika uchaguzi huo.Tume ya kitaifa ya haki za binadamu iliyochunguza tuhuma za kukiukwa haki za binadamu, hata hivyo, ilipigwa marufuku kuangalia uchaguzi.

Mbali na vita vya Tigray, uchaguzi mwaka huu unafanyika huku uchumi wa taifa hilo ukikumbwa na changamoto tele.

Bei ya bidhaa inaendelea kupanda, thamani ya sarafu ya Biir imedorora ikilinganishwa na dola ya Amerika.

Uchaguzi wa mwaka huu pia unafanyika huku baadhi ya wanasiasa waliomezea mate viti vya kisiasa wakiwa wametupwa jela kwa madai ya kuchochea vurugu katika maneneo kadhaa nchini. Mmoja wa wagombea anawania wakati akiwa gerezani.

You can share this post!

Raila akosoa ushuru wa juu unaotozwa wawekezaji

Msajili ajitenga na kashfa ya usajili vyamani