• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
DOUGLAS MUTUA: Haji asihofie ugumu wakazi, aendelee kujitahidi

DOUGLAS MUTUA: Haji asihofie ugumu wakazi, aendelee kujitahidi

Na DOUGLAS MUTUA

MCHAKATO wa sheria hujikokota polepole kiasi cha kumtamausha mtu, lakini hatimaye safari hiyo hufika kituoni inakotarajiwa kuishia.

Hivyo basi, inashangaza kumsikia Mkurugenzi wa mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji, akilalamika kwamba kesi zinacheleweshwa mahakamani na washukiwa wajanja.

Bw Haji amelalamika kwamba pindi anapowasilisha kesi za ufisadi mahakamani, washukiwa wenye nguvu na mamlaka hutumia mbinu za kisheria kuzichelewesha.

Alilalamika hivyo hivi majuzi alipoongoza ujumbe wa heri njema kumtembelea Jaji Mkuu mpya, Bi Martha Koome, ofisini mwake, kitendo cha kiungwana tu miongoni mwa wataalamu wenza.

Kwa maoni yangu, mradi mbinu zinazotumika ni za kisheria, hakuna tatizo lolote. Ikiwa tutaanza kusikiza kilio cha kila anayeteuliwa DPP, basi tutalazimika kuandika katiba mpya mara kwa mara.

Bw Haji alipewa wadhifa anaoshikilia wakati huu kwa sababu iliaminika kwamba angeweza kuyatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Wala ufanisi huo haukutarajiwa kupatikana bila ugumu wa kazi yenyewe, hivyo Bw Haji anapolalamika anatupa hisia kwamba kazi imeanza kumshinda.

Tuelewane kwanza: Binafsi ninakubaliana na Wakenya wengi kwamba kesi za watu wa tabaka la chini zinaharakishwa sana, ghafla unasikia mwizi wa kuku kafungwa miaka miwili.

Hayo yanaendelea huku matajiri na wanasiasa wanaoshukiwa ama kuua watu au kuiba mali ya umma wakiendelea kufurahia uhuru wao kana kwamba hawakutenda kosa lolote.

Masikioni pa mwananchi wa kawaida, malalamiko ya DPP yanasikika kama wimbo mtamu unaopaswa kurudiwarudiwa ili msikilizaji atumbuizwe kikamilifu.

Hata hivyo, uhalisia wa mambo ni tofauti. Ninasema hivi kwa sababu niliripotia gazeti hili kutoka mahakamani kwa miaka kadha.

Ukipata ufahamu wa mambo yanavyokwenda katika idara ya mahakama, jinsi mchakato mzima unavyojikokota, basi unaelewa kilio cha DPP hakina tija.

Alipendekeza Bi Koome abadili jinsi kesi za ufisadi zinavyoshughulikiwa, eti ziwe na kikomo cha muda ambao zinapaswa kushughulikiwa.

Hilo ni pendekezo zuri, lakini hata Bi Koome akidhibiti mambo kiasi cha kuweka kikomo hicho, bado Katiba ina vipengee kadha vinavyomhakikishia mshtakiwa kutendewa haki.

Lengo la Bw Haji ni kuhakikisha kuwa washukiwa wanaofikisha mahakamani hawana muda wa kutosha wa kujitetea au kutumia sheria ili kuepuka adhabu ya faini au kifungo.

Mambo mazuri kweli kwa tabaka la chini linalohisi kama linaonewa, hasa ukiyasikia bila kuyatafakari. Kwa bahati mbaya, Kenya ni taifa lililo na mojawapo ya katiba bora zaidi barani Afrika.

Na ubora huo hautarajiwi kufurahiwa na wanaoongoza mashtaka pekee bali pia wanaopandishwa kizimbani kwa makosa mbalimbali.

Hii ina maana kwamba ile subira ambayo huvuta heri itakuwa muhimu sana kati ya mshtakiwa na upande wa mashtaka.

Ipo falsafa inayosema iwapo jaji au hakimu hana hakika, ni heri kuwaachia huru watu wengi walio na hatia badala ya kumwadhibu mmoja asiye na hatia.

Falsafa hiyo, hata tukibadili katiba mara ngapi, itasalia msingi imara wa utendaji haki katika idara ya mahakama.

Pendekezo la Bw Haji linasikika kama la mtu aliyelemewa na majukumu aliyopewa, hivyo anatafuta njia za mkato za kujirahisishia kazi.

Anapaswa kuelewa kuwa ufanisi wa idara nzima ya sheria hautapimwa tu kutegemea idadi ya washtakiwa watakaoadhibiwa baada ya ofisi yake kuwashtaki.

Wala haipaswi kuchukuliwa kuwa mynonge ananyanyaswa – na tajiri anapendelewa – kwa sababu kesi ya mnyonge inaamuliwa haraka na adhabu kutolewa mara moja.

Kwamba maskini hana pesa za kulipa wakili na hivyo basi kesi yake inasikizwa haraka haina maana ati tajiri aliye na uwezo huo anapendelewa na idara ya mahakama.

Tunapaswa kufahamu na kuzingatia uhalisia wa mambo kabla ya kulalamika na kuonyesha udhaifu wetu hadharani.

[email protected]

You can share this post!

Safari Rally balaa!

LEONARD ONYANGO: Watoto wa mitaani wasidhulumiwe kwa jina...