LEONARD ONYANGO: Watoto wa mitaani wasidhulumiwe kwa jina la kusafisha mji

Na LEONARD ONYANGO

WATOTO wa mitaani, almaarufu chokoraa, wanaorandaranda katikati mwa jiji la Nairobi, Jumatano jioni, walijipata pabaya baada ya kusakwa na kuchapwa viboko na watu waliosadikiwa kuwa maaskari wa Kaunti ya Nairobi.

Watoto hao walikuwa wakichapwa na watu hao huku umati wa watu ukitazama bila kuwasaidia labda kwa sababu chokoraa wanachukuliwa kuwa watoto wasio na thamani.

Waliokuwa wakitekeleza unyama huo, ambao nilishuhudia, hawakuwa wamevaa sare, hivyo ilikuwa vigumu kujua ikiwa walikuwa maaskari (kanjo) wa Kaunti ya Nairobi au la.

Ikiwa watu hao walikuwa maafisa wa serikali ya Kaunti ya Nairobi, basi, aliyetoa amri hiyo anafaa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua kali ya kisheria.

Machokoraa wamekuwa wakidhulumiwa kwa miaka mingi, hasa na maaskari wa kaunti mbalimbali nchini, lakini wanaotekeleza unyama huo hawaadhibiwi.

Wanawafanyia watoto hao uhayawani wanaotaka na kuendelea na maisha yao ya kawaida kana kwamba hakuna ubaya wowote waliofanya.Mnamo 2015, kwa mfano, Rais wa Amerika Barack Obama alipozuru Kenya, serikali ya Kaunti ya Nairobi, iliyoongozwa na Dkt Evans Kidero, wakati huo, ilikusanya chokoraa jijini Nairobi na kuwaficha ‘wasichafue’ jiji.

Serikali ilificha watoto hao ili kufurahisha Rais Obama ambaye msafara wake haukupitia katikati ya jiji alipokuwa nchini.Rais Obama alipokamilisha ziara yake ya siku mbili, watoto hao waliachiliwa huru wakarejea mitaani.

Mnamo 2019, serikali ya Kaunti ya Nakuru ilifurusha watoto wa mitaani 41 usiku na kuwapeleka katika eneo la Chemasusu, Kaunti ya Baringo.

Kufikia sasa watoto watano miongoni mwa hao hawajulikani waliko na suala hilo limefikishwa mbele ya kamati ya Seneti ambapo Gavana Lee Kinyanjui na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu George Kinoti wamelikwa kujibu maswali.

Kuwadhulumu chokoraa kwa kuwachapa au kuwapeleka misituni hakutamaliza changamoto ya watoto wanaorandaranda mitaani katika miji ya Kenya.Wengi wa watoto hao wanajipata mitaani si kwa kupenda kwao bali hali isiyoweza kuepukika.

Baadhi yao ni mayatima na wengine wanasukumwa mitaani na umaskini.Baadhi yao wanaenda mitaani kwa sababu wananyanyaswa na kudhulumiwa nyumbani.

Serikali za kaunti na kitaifa zinafaa kuweka utaratibu mwafaka wa kusaidia watoto hao badala ya kuwaongezea maumivu na mahangaiko.

Watoto hao wanahitaji chakula, elimu bora na makazi mazuri sawa na watoto wengineo wakiwemo wa mabwanyenye au makanjo wanaowadhulumu.

Sharti tayathamini maisha bila kujali tabaka la mtu tusije tukajilitea mikosi kwa matendo yetu yasiyozingatia ubinadamu.