• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
NYABOLA: Vyama vilikiuka sheria ya faragha-data, viadhibiwe

NYABOLA: Vyama vilikiuka sheria ya faragha-data, viadhibiwe

Na NANJALA NYABOLA

WAKENYA walipigwa na butwaa walipogundua kwamba wamesajilishwa na vyama vya kisiasa bila ya wao kujua au kuridhia.

Kashfa iligundulika baada ya Mkenya mmoja kubaini kwamba alipotafuta data zake katika mtandao wa Afisi Maalum ya Usajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP), alikuwa amesajiliwa na chama ambacho hakukitambua.

Mwananchi huyu alitangaza habari hii kwenye mtandao wa Twita, na wengi wetu tukaenda kwenye kurasa za e-Citizen na ORPP kuona kama sisi pia tumeathirika.

Lo! Wengi wetu tulisajiliwa katika vyama vya kisiasa bila kufahamu au kukubali kwetu.

Hili ni jambo la kuudhi sana. Kuna sheria nyingi zilizovunjwa na mtu au watu waliosimamia tukio hii.

Kwanza, kule kugawa data ya wananchi bila kufahamu au kukubali kwao; jambo hili lilipigwa marufuku na katiba pamoja na sheria ya faragha-data ya 2019.

Kwenye sheria za Kenya, usiri ni moja ya haki za binadamu inayolindwa na sehemu 31 ya katiba ya Kenya.

Sheria ya faragha-data inaunganisha kanuni mbalimbali kuhusu ufiche na ufaragha wa data ya wananchi, hasa ikilenga mashirika na serekali yenyewe.

Kulingana na sheria hii, mashirika ya kibinafsi na ya serekali hayaruhusiwi kukusanya, kutumia au kusambaza data ya wananchi zaidi na inayotakikana kuendeleza kazi yao, na bila kufahamu au kukubali kwao.

Kanuni hizi zinaunganishwa na msingi mmoja – kwamba kila mwananchi ana haki ya kulinda data yake nayo serikali ina jukumu la kulinda data yetu dhidi na matumizi mabaya.

Licha ya hayo, inaonekana kwamba walioathiriwa na mgogoro huu walijumuishwa katika vyama vya kisiasa kulingana na makabila yao. Yaani, kwa kuzingatia majina yao au data iliyokusanywa katika vitambulisho vyao, waliwekwa katika chama kinachoambatana zaidi na anayejitambulisha kama kiongozi wake wa kikabila.

Kwa hivyo, Waluhya wengi walipata kwamba wamesajiliwa na chama cha Amani National Congress (ANC) kinachosimamiwa na Musalia Mudavadi. Nao Wakikuyu walijumuishwa katika chama cha Jubilee, na Waluo katika chama cha ODM.

Hii ni kusema kwamba mtandao ulibainisha makabila ya watu kwa kutumia tu data iliyokusanywa na vitambulisho vyetu.

Hali hii ya mambo inadhoofisha azma ya kukomesha ukabila katika siasa nchini kwani desturi hiyo inadhihirisha kuwa kabila pekee ndilo linalofafanua maoni yetu ya kisiasa.

Watalaam wa teknolojia wanadhani kwamba kilichotendeka ni kuwa serikali iligawa data ya wananchi baina ya Kamati Huru ya Uchaguzi (IEBC) na mtandao wa e-Citizen.

E-Citizen ilibuniwa kulainisha shughuli za kiserikali, kwa mfano kuchukua pasipoti, vitambulisho, na leseni za kuendesha magari.

Mtandao huu unakusanya data kadhaa kutoka kwa wananchi, lakini sheria inapiga marufuku kule kugawa au kuuza data hii au kuitumia kwa namna isiyoruhusiwa.

Hata hivyo e-citizen yenyewe si mtandao wa kiserikali, bali ni kampuni binafsi inayopokea hela kutoka kwa serikali ili kusimamia huduma hizi zote.

Kwa hivyo, kashfa hii ni mfano wa matumizi mabaya ya data ya wananchi yaliyopigwa marufuku na sheria ya faragha data ya 2019.

Katika nchi nyingine, hali hii ya mambo ingekuwa aibu kubwa kwa serikali kwani inaonyesha kwamba serikali yenyewe imekosa kulinda sheria zake zenyewe.

Lakini wasimamizi wa ORPP wameteta kwamba ni jukumu la Wakenya kujiondoa katika orodha za vyama vya kisiasa, hata kama Wakenya haohao wanapinga kwamba hawakujisajilisha; kwa nini iwe kazi yao kujiondoa?

Zaidi ya hayo, hasa katika nchi yetu, kashfa hii inatisha kwani ukabila ni mojawapo wa pingamizi dhidi ya umoja na maendeleo nchini.

Ni muhimu sana kwamba wananchi wawe na imani katika mashirika yanayosimamia uchaguzi, hususan katika nchi kama Kenya ambamo uchaguzi huleta vita.

Kwa kutofuata sheria ya faragha-data na usiri, Afisi ya Usajili wa Vyama vya Kisiasa imeleta utatanishi siasani ambayo imeshazoroteka sana kabla ya uchaguzi wa 2022.

Wakenya sasa wana wasiwasi kwa sababu serikali ya Kenya inatuonyesha kwamba haijajifunza lolote kutokana na uchaguzi wa 2017. Katika uchaguzi huo tuliona tena kuwa data ya wananchi ilitumiwa kuwasajili katika vyama bila kujua au kukubali kwao.

Tuliona kwamba matumizi mabovu ya teknolojia na data ilileta utatanishi na sintofahamu nchini.

Inaonyesha kwamba mashirika ya serikali bado hayajafahamu vyema kwamba faragha data sio huria bali ni ya lazima.

Aidha, faragha data ni mojawapo ya haki za kidijitali, na ni muhimu kuilinda vyema katika harakati za kuimarishia demokrasia nchini.

Nyabola ni Mwandishi, Mtafiti na Mchanganuzi wa Siasa

You can share this post!

Uchaguzi 2022 ni lazima – Ruto

Madaktari na maafisa bandia wa mifugo Kiambu kuadhibiwa...