• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Madaktari na maafisa bandia wa mifugo Kiambu kuadhibiwa vikali – Nyoro

Madaktari na maafisa bandia wa mifugo Kiambu kuadhibiwa vikali – Nyoro

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kiambu James Nyoro ametoa onyo kali kwa madaktari na maafisa bandia wa mifugo wanaohangaisha wafugaji na wakulima.

Bw Nyoro amesema maafisa tapeli watakaopatikana, serikali yake haitakuwa na budi ila kuagiza wakamatwe na kufunguliwa mashtaka.

“Lazima wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake. Ifahamike wazi kuwa wanaopaswa kuhudumu ni waliofuzu na kuidhinishwa kupitia asasi husika,” gavana huyo akaambia Taifa Leo.

Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai alitangaza awali kuwa serikali kuu imeweka mikakati maalum kuajiri madaktari wa mifugo katika kila jimbo, ili kusaidia kukabili kero ya maafisa bandia na chakula, madini na bidhaa ghusi za ufugaji.

“Baadaye tutahakikisha kila kaunti inapata inspekta mmoja. Tunataka sekta ya ufugaji nchini iimarike,” Bw Kimtai akasema.

Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai (aliye na mikrofoni) anasema serikali imeweka mikakati kabambe kusadia kukabiliana na kero ya maafisa bandia wa mifugo na bidhaa ghushi za ufugaji. Picha/ Sammy Waweru

Hata ingawa Nyoro anasema anatambua kuwepo kwa maafisa bandia wa mifugo, alisema utendakazi wa huduma za mifugo unapaswa kutekelezwa na serikali za kaunti ila si serikali kuu.

“Kero ya maafisa bandia wa mifugo ni sawa na ile ya madaktari wa binadamu. Shughuli za ufugaji ni jukumu la serikali ya kaunti. Sekta ya kilimo na ufugaji imegatuliwa, chini ya Katiba ya 2010,” akasisitiza.

Gavana huyo alisema serikali ya kitaifa inapaswa kuibuka na sheria na mikakati faafu, itakayofuatwa na serikali za kaunti kuimarisha huduma za ufugaji nchini.

“Tunachoomba serikali kuu, ni kubuni sheria maalum. Kwa mfano, Kiambu ikiweza kudhibiti magonjwa, kisha kaunti zingine zikose, au zingine zifanikiwe Kiambu ilegee, hatutapiga hatua zozote mbele kuboresha huduma za ufugaji,” akafafanua.

You can share this post!

NYABOLA: Vyama vilikiuka sheria ya faragha-data, viadhibiwe

Mpango wa Crystal Palace kuajiri kocha Lucien Favre wagonga...