• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:25 PM
Wanafunzi 30 wapokea ufadhili kutoka kwa MKU

Wanafunzi 30 wapokea ufadhili kutoka kwa MKU

LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wapatao 30 kutoka Shule ya Msingi ya Kamenu mjini Thika wamenufaika na ufadhili kutoka kwa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU).

Wanafunzi hao wanaotarajia kujiunga na shule za upili ni baadhi ya waliopita vizuri mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE).

Msimamizi wa kitengo cha masomo katika chuo hicho Bw Emmanuel Owuor alisema wanafunzi hao ni miongoni mwa wale waliopata alama za kuridhisha.

Alieleza kuwa wanafunzi hao walipokea masanduku, vitabu, na sabuni ikiwa ni njia moja ya kuwapunguzia wazazi mzigo wa kununua vifaa vya shule.

Hafla hiyo iliyofanyika MKU mnamo Jumamosi ilihudhuriwa na wazazi wa wanafunzi hao.

Baada ya kupokea vifaa hivyo wanafunzi hao walihamasishwa kwa kushauriwa wawe watiifu kwa walimu wao na wazingatie masomo yao kwa kutia bidii.

“Nyingi kama wanafunzi mnastahili kuwa na nidhamu na kusoma kwa bidii ili kuafikia malengo yenu,” akasema Bw Owuor.

Wazazi wao walipongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na MKU wakiitaja kama ya manufaa kwao.

Bw Owuor aliwajulisha wazazi kuwa MKU itakuwa mstari wa mbele kufuatilia masomo ya wanafunzi hao.

“Wazazi pia ni sharti muwe mstari wa mbele kuona ya kwamba watoto wenu wanaendeleza masomo yao jinsi ipasavyo,” akafafanua Bw Owuor.

MKU kwa muda mrefu imekuwa ikifadhili miradi tofauti ikiwemo kufanikisha utoaji wa matibabu ya bure kwa wakazi wa kijiji cha Kiandutu kilichoko mjini Thika.

You can share this post!

Manchester City kumsajili Griezmann iwapo mpango wao wa...

Kiunjuri aonya Rais asijiongeze muda