• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Chai: Bomet yapata soko Iran

Chai: Bomet yapata soko Iran

Na KENYA NEWS AGENCY

SERIKALI ya Kaunti ya Bomet kwa ushirikiano na kampuni za eneo hilo itauza majanichai yanayokuzwa kaunti hiyo moja kwa moja nchini Iran, ili kuwezesha wakulima kupata faida.

Akihutubu alipoanzisha usafirishaji wa tani 84 za majanichai kutoka kampuni za kibinafsi, Gavana wa Bomet, Bw Hillary Barchok alisema Kaunti hiyo imepata idhini kutoka kwa Wizara ya Kilimo kuuza zao hilo nchini Iran.

Alisema utawala wake umejitolea kusaidia katika mauzo ya majanichai yanayotayarishwa na viwanda vilivyoko Bomet ili kuimarisha bei kwa manufaa ya wakulima na kampuni hizo za kibinafsi.

“Tutazisaidia kampuni za umma na za kibinafsi kufikia soko za ng’ambo kwa sababu hapa Bomet hatuna kampuni za kuongeza thamani kwa zao la chai,” Bw Barchok akasema.

Gavana huyo, ambaye alikuwa ameandamana na Balozi wa Iran nchini, Jafar Barmaki alisema licha ya mpango huo kukabiliwa na changamoto nyingi ana matumaini kuwa utafaulu.

Akirejelea Sheria mpya ya Chai yenye kipengele kinachopiga marufuku uuzaji zao hilo moja kwa moja, Bw Barchok alipongeza mahakama kwa kukubali kesi yake inayopinga kipengele hicho.

“Tuko hapa kuanzisha usafirishaji wa shehena ya kwanza ya majanichai inayopelekwa moja kwa moja hadi Iran, kwa sababu mahakama ilikubaliana na ombi letu. Tulitaka utekelezaji wa kipengele kinachozima uuzaji majanichai moja kwa moja usimamishwe ili tuweze kuuza zao hili kwa bei nzuri kwa manufaa ya wakulima wadogo,” akaeleza.

Gavana Barchok alisema kuna jumla ya wakulima wadogo 100,000 katika Kaunti ya Bomet ambao wamekuwa wakinyanyaswa na wanunuzi wa zao hilo humu nchini. Aliongeza kuwa wakulima hao hawajafaidi chini ya mpango wa majanichai kuuzwa na Shirika la Ustawishaji Majani Chai Nchini (KTDA) na kupitia mnada wa Mombasa.

“Mkataba ambao tumetia saini na Iran unaanza kutekelezwa kuanzia leo (Ijumaa) na nina imani kuwa wakulima wetu watafaidi pakubwa,” akasema

Gavana Barchok pia alifurahishwa na hali kwamba mkataba huo wa kibiashara umepata uungwaji mkono kutoka kwa asasi husika za serikali, na kuiwezesha Bomet kuanzisha usafirishaji wa zao hilo.

Alisema baada ya kuanza na tani 84, serikali yake ina matumaini kwamba kufikia mwaka ujao watakuwa na uwezo wa kuuza tani 100 za majani chai nchini Iran.

Kwa upande wake balozi wa Iran, Barmaki, alipongeza Kaunti ya Bomet kwa kufanikisha mpango huo.

Nao wakulima wakiongozwa na Bw John Terer alisema mpango wa uuzaji chai moja kwa moja nchini Iran ni mwamko mpya katika kilimo cha zao hilo.

Terer alisema ukiritimba wa KTDA na wadau wengine unafaa kudhibitiwa kwa manufaa ya wakulima.

You can share this post!

Magavana 3 wa Pwani mbioni kujijengea jina

Waziri ajiuzulu kufumaniwa akibusiana na msaidizi wake