• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Uhispania waingia robo-fainali za Euro baada ya kuangusha Croatia katika muda wa ziada

Uhispania waingia robo-fainali za Euro baada ya kuangusha Croatia katika muda wa ziada

Na MASHIRIKA

UHISPANIA walitinga robo-fainali za Euro mnamo Jumatatu usiku baada ya kudengua Croatia kwenye hatua ya 16-bora kwa mabao 5-3 katika muda wa ziada jijini Copenhagen, Denmark.

Ushindi huo wa Uhispania uliwakatia tiketi ya kuvaana na Uswisi kwenye robo-fainali baada ya Uswisi kuwang’oa mabingwa wa dunia Ufaransa kwa penalti 5-4.

Chini ya kocha Luis Enrique, chombo cha Uhispania kiliyumbishwa na Croatia waliotoka nyuma kwa mabao 3-1 na kufunga mabao mawili chini ya dakika tano za mwisho wa muda wa kawaida na kulazimisha gozi hilo kuingia muda wa ziada wa dakika 30.

Magoli hayo yaliyorejesha Croatia mchezoni yalifumwa wavuni kupitia Mislav Orsic na Mario Pasalic katika dakika za 85 na 90.

Awali, Pablo Sarabia, Cesar Azpilicueta na Ferran Torres walikuwa wamewaweka Uhispania kifua mbele kufikia dakika ya 76 baada ya Pedri Gonzalez wa Uhispania kujifunga katika dakika ya 20 na kuwapa Croatia motisha ya kutatiza zaidi kipa Unai Simon.

Fowadi Alvaro Morata aliyekuwa ameeleza hofu ya kutishiwa maisha na mashabiki baada ya kupoteza nafasi nyingi za kufungia Uhispania katika mechi za awali, alinyamazisha wakosoaji.

Fowadi huyo anayechezea Juventus kwa mkopo kutoka Atletico Madrid, alifunga bao la nne la Uhispania katika dakika ya 100, sekunde chache kabla ya Mikel Oyarzabal kuzamisha kabisa chombo cha Croatia.

Ilikuwa mara ya pili mfululizo kwa Croatia waliokuwa wanafainali wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, kubanduliwa kwenye hatua ya 16-bora kwenye Euro. Kikosi hicho cha kocha Zlatko Dalic kilidenguliwa pia na Ureno kwenye hatua ya 16-bora ya Euro mnamo 2016 nchini Ufaransa.

Croatia walifungua kampeni za Kundi D kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Uingereza kabla ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Czech na kulaza Scotland 3-1 hatimaye.

Uhispania kwa upande wao walitawazwa mabingwa wa Euro mnamo 1964, 2008 na 2012; na wakaibuka wafalme wa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini. Walicharaza Slovakia 5-0 katika mchuano wa mwisho wa Kundi E baada ya kulazimishiwa sare tasa na ya 1-1 dhidi ya Uswidi na Poland kwenye mechi mbili za ufunguzi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uswisi wadengua vigogo Ufaransa na kujikatia tiketi ya...

Kocha Scott Parker aondoka Fulham na kuyoyomea Bournemouth