• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 2:18 PM
TSC yafungua roho kwa Knut baada ya Sossion kuondoka

TSC yafungua roho kwa Knut baada ya Sossion kuondoka

Na DAVID MUCHUNGU

SIKU mbili baada ya Wilson Sossion kujiuzulu kama Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut), Tume ya Huduma za Walimu (TSC) sasa imeonyesha nia ya kutaka kurejesha uhusiano bora kati yake na chama hicho.

Jumatatu, TSC ilialika vyama vya kutetea masilahi ya walimu, ikiwemo Knut, kwa mazungumzo kuhusu nyongeza ya mishahara.

TSC imeitisha mkutano huo wa kujadili mkataba mpya kuhusu nyongeza ya mishahara (CBA) licha ya Tume ya Mishahara (SRC) kuahirisha nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutokana na makali ya janga la Covid-19.

Kuanzia Jumanne, Juni 29, 2021, Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia, atafanya mazungumzo na vyama vya Knut, Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo (Kuppet) na Chama cha Walimu wa Shule za Wanafunzi wenye mahitaji Maalum (KUSNET) kujadili CBA ya kipindi cha 2021-2025.

Kulingana na barua ya mwaliko kwa vyama hivyo, TSC itawasilisha mapendekezo yake kuhusu nyongeza ya mishahara. Ofa hiyo ndiyo itajadiliwa katika mazungumzo hayo.

Tayari vyama vimewasilisha mapendekezo yao kuhusu nyongeza ya mishahara kwa TSC. Kuna jumla ya walimu 330,671 kwenye sajili ya TSC ambao hulipwa mishahara na tume hiyo.

Mei, vyama vya kutetea masilahi ya walimu hao vimekuwa vikiomba kufanya mazungumzo na TSC kuhusu suala hilo la nyongeza ya mishahara.

Barua ya TSC ya kuvialika vyama hivyo kwa mazungumzo ilitumwa mnamo Juni 25, 2021 siku ambayo Bw Sossion alijiuzulu kabla ya uchaguzi wa Knut kufanyika katika uwanja wa Ruaraka, Nairobi.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

TAHARIRI: Viongozi wasiijadili kesi ya rufaa ya BBI

WANGARI: Mageuzi katika sekta ya kilimo yazingatie pia...