• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
WASONGA: Ripoti kuhusu utendakazi wa wabunge ina mianya mingi

WASONGA: Ripoti kuhusu utendakazi wa wabunge ina mianya mingi

Na CHARLES WASONGA

MAJUKUMU makuu ya wabunge ni utungaji sheria, uwakilishi na uchunguzi wa utendakazi wa serikali kuu inayoongozwa na Rais.

Vile vile, wawakilishi hao wa wananchi hutekeleza wajibu muhimu kuandaa bajeti ya kitaifa kwa ushirikiano na Hazina ya Kitaifa.

Wao pia huamua ugavi wa fedha kati ya ngazi mbili za serikali; Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti. Wabunge pia wana wajibu wa kupitisha hoja ya kuidhinisha vita kati ya Kenya na taifa hasimu na hoja za kuwatimua mamlaka Rais, Naibu wake na Mawaziri.

Kwa upande wa maseneta, wajibu wao mkuu kulingana na kipengele cha 96 cha Katiba ni kutetea na kulinda masilahi ya serikali za kaunti na kutunga sheria zinazolenga kufanikisha utawala wa ugatuzi.

Maseneta pia hukadiria viwango vya ugavi wa fedha, za bajeti, miongoni mwa serikali 47 za kaunti. Wao pia huchunguza utendakazi wa maafisa wakuu wa serikali kuu.

Kimsingi, sehemu kubwa ya majukumu ya wabunge na maseneta hutekelezwa katika kamati za kila bunge kwa sababu mabunge hayo hufanya vikao siku tatu pekee kwa wiki.

Vikao vya kamati pia huwa ni majukwaa faafu kwa wabunge na maseneta kuchangia miswada na hoja pamoja na kuchambua masuala mengi yanayowahusu wananchi kuliko vikao vikuu ambavyo hubanwa na muda na idadi kubwa ya wanaohudhuria. Maelezo haya yanalenga kukosoa ripoti ya Shirika la Mzalendo inayotoa dhana kwamba wabunge wasiozungumza mara nyingi bungeni ni wazembe. Hii ni licha ya kwamba, wao hutia kibindoni mamilioni ya fedha kama mishahara na marupurupu.

Kulingana mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, maafisa wake wafuatilia michango ya wabunge na maseneta katika vikao vya wabunge wote pekee wala sio katika kamati ambako zaidi ya asilimia 80 ya majukumu ya wawakilishi hao wa raia huendeshwa. Hatimaye Mzalendo Trust iligundua jumla ya wabunge na maseneta 34 hawakutamka lolote mwaka jana, 2020.

Sisemi hamna wabunge na maseneta wazembe na ambao huwa hawachangii lolote hata katika vikao vya kamati. Wapo; na baadhi yao wameorodheshwa kwenye ripoti ya Mzelendo Trust iliyotolewa Jumatatu.

Lakini tasnifu yangu ni kwamba, ripoti za shirika hilo, ambalo hufuatilia utendakazi wa wabunge, zingekuwa na mashiko na manufaa kwa umma, endapo zingenasa pia michango ya wabunge na maseneta katika kamati za mabunge yote mawili.

Ripoti yake ya hivi punde, na zingine za hapo nyuma, zinazomulika utendakazi wa wabunge kwa misingi ya yale waliyosema katika vikao vikuu, hazitoi tathmini sahihi ambayo wananchi wanaweza kutumia kubaini manufaa ya wawakilishi wao.

[email protected]

You can share this post!

Tuju adai ‘Tangatanga’ wamechoka

NGILA: Kamera za kidijitali zitapiga vita ujangili, ukataji...