• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
NGILA: Kamera za kidijitali zitapiga vita ujangili, ukataji wa miti

NGILA: Kamera za kidijitali zitapiga vita ujangili, ukataji wa miti

Na FAUSTINE NGILA

HATUA ya kampuni moja ya Amerika kuwekeza kwenye teknolojia ya kuisaidia Kenya katika vita dhidi ya ujangili imefika kwa wakati unaofaa hasa kwa Wizara ya Utalii.

Kampuni ya Flir Systems imetoa kamera za dijitali zenye thamani ya Sh300 milioni zenye uwezo wa kunasa picha za mbugani katika hali yoyote ya anga, iwe usiku au mchana.

Mbuga kumi za hapa nchini zinatazamiwa kufaidika kwa mpango huu unaolenga kulinda wanyamapori wote na kuwanasa majangili.

Hii ni ithibati nyingine kuwa teknolojia itazidi kutumika kuleta suluhu kwa changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi tunazokumbana nazo.

Na kwa kila teknolojia, watumizi wapya hufunzwa jinsi ya kuitumia, na sasa maafisa wa usalama kwenye mbuga watafundishwa jinsi ya kunasa wawindaji haramu wa usiku.

Katika Mbuga ya Maasai Mara ambapo teknolojia hii ilifanyiwa majaribio miaka miwili iliyopita, wawindaji haramu 160 walikamatwa.

Hii ni teknolojia inayowezesha kamera kuona wazi wakati kuna giza, moshi au vumbi na itasaidia pakubwa kupunguza idadi ya ndovu na vifaru wanaouawa mbugani.

Wizara ya Utalii sasa inafaa kujitwika jukumu la kuhakikisha teknolojia hii imetumika katika mbuga zote za Kenya huku ile ya Mazingira nayo ikihakikisha imeitumia kuwatia nguvuni wale walio na mazoea ya kukata miti kiholela ili kudumisha hadhi ya misitu yetu.

Uchomaji makaa umekuwa kero katika vita dhidi ya kawi chafu nchini, huku baadhi ya wananchi wakijificha usiku na kukata miti bila kutambuliwa.

Iwapo kamera hizi za kisasa zitawekwa katika maeneo mbalimbali ya misitu na mbuga, watu wengi watanaswa na kushtakiwa. Hatua hii itaogofya wengine wenye nia sawa, na hatimaye utalii wetu utapanuka zaidi na kutufaa kama taifa.

Hivyo, serikali kivyake bila ufadhili inafaa kuvalia njuga teknolojia hii, na kuwekeza katika ununuzi wa kamera hizo ili maafisa zaidi wa kukabiliana na uwindaji haramu wapewe mafunzo pamoja na wale wa Shirika la Huduma za Misitu nchini.

Ikumbukwe kuwa, mwaka 2020 ripoti moja ilifichua kuwa ndovu 26 waliuawa katika mbuga ya Maasai Mara katika kipindi cha miezi mitatu kwa kunyweshwa sumu.

Kwa kutumia kamera hizi, itakuwa rahisi kubaini waliotenda unyama huo wa kujaribu kulemaza juhudi zinazofanywa na Bodi ya Kitaifa ya Utalii kuvumisha sekta ya utalii Kenya.

Iwapo Wizara ya Utalii na ile ya Mazingira zitakumbatia teknolojia hii, ujangili na ukiukaji wa marufuku dhidi ya ukataji miti nchini Kenya utakomeshwa.

Lakini iwapo serikali itazidi kutegemea ufadhili na msaada wa mataifa ya nje, basi changamoto nyingi zinazosuluhishwa na teknolojia zitazidi kuumiza uchumi wetu.

La muhimu ni kujifunza kutokana na ubunifu huo wa Amerika na kuwapa nafasi wataalamu wetu wa teknolojia kuvumbua mbinu zinazosaidia taifa hili kupiga hatua kiuchumi.

You can share this post!

WASONGA: Ripoti kuhusu utendakazi wa wabunge ina mianya...

NDIVYO SIVYO: Tofauti katika matumizi ya vikanushi...