Uingereza pazuri kutinga fainali ya Euro baada ya kudengua Ujerumani

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walifunga katika dakika za mwisho na kusajili ushindi wa 2-0 uliowasaidia kubandua Ujerumani kwenye hatua ya mwondoano ya soka ya haiba kubwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 55.

Ushindi huo wa Uingereza uliowasisimua maelfu ya mashabiki wao uwanjani Wembley, uliwapa fursa maridhawa zaidi ya kutia kapuni taji la Euro mwaka huu.

Chini ya kocha Gareth Southgate, Uingereza kwa sasa watavaana na Ukraine kwenye robo-fainali huku mshindi wa mechi hiyo akikutana ama na Jamhuri ya Czech au Denmark kwenye nusu-fainali.

Raheem Sterling wa Manchester City aliwaweka Uingereza kifua mbele katika dakika ya 75 kabla ya nahodha Harry Kane wa Tottenham Hotspur kuzamisha kabisa chombo cha Ujerumani.

Mechi hiyo ilikuwa ya mwisho kwa mkufunzi Joachim Loew kusimamia kambini mwa Ujerumani. Mikoba ambayo amekuwa akidhibiti kwa miaka 15 iliyopita sasa itatwaliwa rasmi na kocha wa zamani wa Bayern Munich, Hansi Flick.

Bao la Sterling lililochangiwa na beki Luke Shaw, lilikuwa lake la tatu kwenye kampeni za Euro mwaka huu. Fowadi huyo wa zamani wa Liverpool alipachika wavuni mabao mawili mengine katika hatua ya makundi – moja dhidi ya Croatia na jingine dhidi ya Jamhuri ya Czech.

Goli la pili la Uingereza lilikuwa zao la ujio wa kiungo Jack Grealish aliyeongeza kasi katika safu ya mbele iliyomtatiza pakubwa kipa Manuel Neuer wa Ujerumani. Timo Werner, Kai Havertz na Thomas Muller walipotezea Ujerumani nafasi kadhaa za wazi katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Uingereza walikamilisha kampeni zao za Kundi D kileleni baada ya kushinda Croatia 1-0, kuambulia sare dhidi ya Scotland na kupokeza Jamhuri ya Czech kichapo cha 1-0.

Kwa upande wao, Ujerumani ambao ni mabingwa mara tatu wa Euro (1972, 1980, 1996) walishuka dimbani baada ya kuchapwa 1-0 na Ufaransa kabla ya kucharaza Ureno 4-2 na kulazimishiwa na Hungary sare ya 2-2 katika Kundi F.

Hadi Jumatano, Ujerumani waliwahi kupepeta Uingereza 6-5 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1 kwenye nusu-fainali ya Euro mnamo 1996.

Ili kudhibiti kasi ya mafowadi wa Ujerumani, Southgate alikumbatia mfumo wa 4-2-3-1 uliowavunia Uingereza ushindi dhidi ya Croatia katika hatua ya makundi.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Uingereza kulaza Ujerumani chini ya dakika 90 kwenye hatua ya muondoano ya Euro. Hata hivyo, ilidhihirika kwamba makali yaliyojivuniwa na Ujerumani miaka saba iliyopita walipotwaa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil yameshuka.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO