• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mwanataekwondo Ogallo ashinda uandishi wa insha ya Olimpiki Kenya

Mwanataekwondo Ogallo ashinda uandishi wa insha ya Olimpiki Kenya

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Faith Ogallo si mchache tu katika mchezo wa taekwondo! Ogallo, ambaye atawakilisha Kenya kwenye Olimpiki katika mchezo wa taekwondo mjini Tokyo, Japan, ameshinda mashindano ya siku ya Olimpiki (kitengo cha kuandika insha) mnamo Juni 30.

Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K) imetangaza kuwa mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kibabii katika Kaunti ya Bungoma pamoja na BettyLily Karoki na Baraka Munyua (Nairobi) na Lorence Ishuga kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta waliibuka washindi kwa kuandika insha.

Mashindano hayo pia yalikuwa na kitengo cha uchoraji kilichopata washindi saba. Wachoraji walioibuka na ushindi ni Saanya Deepesh Shah kutoka Oshwal Academy jijini Nairobi, Marco Larson (Braeburn, Nairobi), Benji Mkenya (St Peter’s Academy, Narok), Sharleen Wanja (Pioneer School, Thika), Ann Achieng (Nembu Girls, Nairobi) na Clinton Osebe na Randy Njuguna (Nairobi School, Nairobi).

Dhamira ya mashindano hayo ilikuwa michezo ya Olimpiki za Tokyo 2020 ikilenga kueneza elimu kuhusu Olimpiki na falsafa ya michezo hiyo.

Mashindano hayo yalikuwa wazi kwa wanafunzi kutoka shule za msingi, sekondari na taasisi za masomo ya juu. Washiriki walihitajika kuwasilisha michoro yao ama insha zao kati ya Juni 23 na Juni 25. Washindi wote walitunukiwa cheti cha kushiriki, vocha na tuzo ya kumbukumbu katika afisi za NOC-K mtaani Westlands.

You can share this post!

Wanafunzi wanane katika kituo cha kurekebisha tabia wapata...

Wanawake Waislamu wataka kuongoza korti za Kadhi