• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 AM
Moto wateketeza afisi ya naibu kamishna Lari, nyumba za polisi

Moto wateketeza afisi ya naibu kamishna Lari, nyumba za polisi

Na LAWRENCE ONGARO

MOTO mkubwa ulishuhudiwa katika eneo la Lari katika wadi ya Kinare, Kaunti ya Kiambu na kuteketeza afisi ya naibu kamishna na nyumba za polisi.

Tayari maafisa wa upelelezi wameanza kufanya uchunguzi kubainisha kiini cha moto huo ulioshuhudiwa mwendo wa saa nne za asubuhi mnamo Jumatano.

Raia walifika hapo kusaidia ili kuzima moto huo ambao hadi sasa hakijulikani chanzo chake.

Naibu Kamishna wa Lari, Bi Agnes Karoki, alieleza kuwa hakuna aliyefariki ama kujeruhiwa kwenye mkasa huo.

“Ninawapongeza wananchi kwa kuonyesha uzalendo wao kwa kuingilia kati kusaidia kuondoa hatari hiyo iliyoshuhudiwa. Nina hakika kila kitu kitaendelea vyema na kazi itarejelea hali ya kawaida,” alieleza Bi Karoki.

Alieleza kwamba maafisa wa upelelezi watafanya uchunguzi ili kubainisha kiini cha moto huo.

Wananchi pia waliiomba serikali kufanya juhudi kuona ya kwamba mambo yanaenda sawa ili hali irekebishwe kwa kujenga nyumba za manufaa kwa wananchi.

Mkazi Bi Ruth Njeri alieleza kuwa wakazi wa kijiji cha Kinare walishtushwa na mkasa huo lakini akasema pia anafurahi kwa sababu kwa ushirikiano wao na maafisa wa serikali, walifanikiwa kuuzima moto huo.

“Ushirikiano wetu kama wakazi wa Lari pamoja na maafisa wa serikali ulisaidia pakubwa hadi moto huo ukazimika. Tuna imani kutakuwa na marekebisho ya kukarabati afisi ya naibu kamishna na nyumba za polisi,” akasema Bi Njeri.

Naye mkazi mwingine, Bw Charles Nyoro, alisema ushirikiano mzuri wa polisi na wananchi utasababisha kujengwa upya kwa kituo hicho ambacho kimeachwa katika hali mbaya.

Wananchi wamependekeza hali ya mazingira ya mahali hapo iangaziwe zaidi kwa sababu eneo hilo limezingirwa na miti mingi.

“Sisi kama wakazi wa hapa tunataka kujengewa kituo kizuri cha polisi ili pia tuwe katika mazingara mazuri,” alisema Bw Nyoro.

Naibu Kamishna atatafutiwa mahali pengine pa kuishi kabla ya kupata makazi ya kudumu.

You can share this post!

Tottenham wampa Nuno Espirito Santo mikoba yao ya ukocha

TAHARIRI: Vyama vya kisiasa viwe na ukomavu