• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Wapigakura wa kulaumiwa kuchagua viongozi wafisadi

KINYUA BIN KING’ORI: Wapigakura wa kulaumiwa kuchagua viongozi wafisadi

Na KINYUA BIN KING’ORI

KATI ya maswala makuu yanayochangia uchumi wa taifa hili kudidimia, ni ufisadi uliokithiri.

Ufisadi umechangia mataifa mengi ulimwenguni kusalia nyuma kimaendeleo.

Nchini Kenya, wananchi hulalamika jinsi viongozi wenye ushawishi mkubwa serikalini kuanzia serikali za kaunti hadi ya kitaifa wanavyotumia mamlaka yao kushiriki ufisadi bila kujali. Maafisa wanaohusika na vitendo vya ufisadi huwa ni wajasiri ajabu. Hawaogopi kuchukuliwa hatua ikiwa itathibitishwa wanashiriki visa vya ufisadi. Yamkini maafisa hao hulindwa na wakubwa wao kazini.

Ufujaji wa fedha za umma umezidi katika idara mbalimbali za serikali na ni rahisi kung’amua kuwa wahusika wakuu ni viongozi walio mamlakani kwa namna wanavyoshughulikia masuala ya ufisadi kwa njia ya uzembe na ubaguzi.

Wananchi pia ni wa kulaumiwa kwa kukumbatia viongozi hasa wanasiasa wanaohusishwa na ufisadi. Aghalabu, wamewafanya mashujaa baadhi ya washukiwa Kwa kuwachagua kushikilia nyadhifa muhimu mashinani kama vile wabunge, maseneta au magavana.

Ukweli ni kwamba, imekuwa vigumu hata Kwa tume ya kupambana na ufisadi nchini kufaulisha vita dhidi ya janga hilo kwa sababu hakuna aliye tayari kujitolea kuwafichua wafisadi.

Si rahisi vita hivi kufaulu ikiwa tume husika na serikali kwa jumla watakosa kuweka mikakati kabambe kuwalinda wananchi jasiri watakaokubali kufichua visa vya ufisadi iwe serikalini au katika mashirika binafsi.

Je, serikali inatarajia kufanikiwa vipi katika vita vya kupambana na ufisadi miongoni mwa maafisa wake ikiwa wananchi wazalendo wanaojitolea kufichua visa vya hivyo hawapewi mazingira salama kutekeleza wajibu huo? Je, ikiwa madai ya kufutwa kazi kwa mzalendo aliyekuwa na ujasiri kufichua uovu na ufisadi uliokumba chuo kikuu cha Maasai Mara ni ya kweli, mbona watu wasiogope kuwafichua maafisa fisadi?

Vita dhidi ya janga la ufisadi vinafaa kutiwa nguvu kwa kuwa na sheria kali inayowaadhibu maafisa watakaofuta wenzao kazi kwa kufichua visa vya ufisadi. Inashangaza kwamba, juhudi za watu wanaofichua njama za ufisadi hazitambuliwi wala kupewa usalama wa kutosha. Wapo watu wenye ushawishi serikalini pia wanaochangia juhudi hizo kulemazwa au kutofanikiwa.

Kwa sasa, miradi mingi yenye manufaa makubwa kwa raia, iwe imeanzishwa na serikali za magatuzi au kitaifa imekwama baada ya fedha zilizotengewa kufujwa. Hii imelazimisha wananchi kuendelea kuumia huku uchumi nao ukidorora.

You can share this post!

KAMAU: Himaya za kifalme hazina nafasi sasa

AKILIMALI: Mkulima anavyochuma kutokana na matundadamu