• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
AKILIMALI: Miaka 20 akizalisha ndizi, zina mapato ila Covid nusra imvuruge

AKILIMALI: Miaka 20 akizalisha ndizi, zina mapato ila Covid nusra imvuruge

Na SAMMY WAWERU

HANNAH Njoki amekuwa katika kilimo cha ndizi kwa zaidi ya miaka 20 na anakiri ni zao lenye mapato ya haraka.

Alikikumbatia ili kusaidia kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kismingi.

Njoki hata hivyo anasema aligeuza wazo hilo kuwa biashara, baada ya majirani na wanakijiji kuridhishwa na mazao yake, na kuomba wauziwe.

“Nilianza na kipande kidogo tu cha ardhi na baada ya kugundua ndizi zina soko, niliongeza hadi ekari mbili,” anasema.

Alitumia mtaji wa Sh10,000 pekee, uliogharamia mbolea na leba, mbegu akipanda migomba asilia.

Hata ingawa baadaye alipunguza hadi ekari moja, Njoki anaendeleza kilimo cha zao hilo katika kijiji cha Gachinga, Ikinu, Kaunti ya Kiambu.

Alichukua hatua hiyo ili kujumuisha mimea mingine, angalau kuona ana mseto wa mazao.

Huku wengi wa wakazi eneo hilo wakijishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ukulima wa mahindi na maharagwe, Njoki amepamba uga wake wa matunda kwa migomba.

Aidha, kuna inayochana maua, kutunda na mingine ndizi kukomaa, mama huyu akisema kila wiki hakosi kufanya mavuno.

“Mavuno yakichelewa sana labda ni kwa mwezi mmoja pekee,” aelezea, akisema ameratibu shamba lake kwa mpangilio.

Kulingana na masimulizi yake, tangu aingilie kilimo cha ndizi, kimekuwa kikimpa tabasamu, furaha ambayo imemrahisishia kusukuma gurudumu la maisha.

Mahangaiko ya kupata karo, ameyaangazia kwa kiwango kikubwa.

“Kimsingi, sijataabika vile kupata karo. Mtoto anapotumwa nyumbani, hufanya mauzo ya ndizi na kumrejesha,” asema mkulima huyu ambaye ni mama watoto wanne.

Ndizi zikiwa miongoni mwa matunda kipenzi cha wengi, Njoki anasema soko bora limekuwa la mazao mabichi.

Aidha, wanunuzi wake wanatoka masoko mbalimbali Kiambu.

Ni kilimo-biashara anachosema kilikuwa kimenoga hadi Kenya ilipokumbwa na janga la corona Machi 2020, mambo yakaanza kuenda mrama.

Njoki anaiambia Akilimali kwamba soko la ndizi limeyumbishwa, kiasi cha kuhofia mazao yake kuozea shambani.

“Kwa sasa nina zaidi ya vifungu 200 vilivyokomaa shambani. Nina wasiwasi visiive kabla sijapata wanunuzi,” anasema.

Bei ya kifungu kimoja, hutegemea udogo au ukubwa wake. Huchezea kati ya Sh200 – 1, 000.

Kinyume na awali, mkulima huyu anasema wateja wake na ambao ni wa kijumla hawanunui mazao kwa wingi, pengine kwa hofu ya kukadiria hasara.

Ugonjwa wa Covid-19, na ambao ni janga la kimaitaifa umeathiri karibu sekta zote, ile ya kilimo na biashara pia ikijumuishwa.

Licha ya serikali kudai soko la mazao mbichi ya kilimo, hasa matunda na maua, limenoga nje ya nchi kipindi hiki cha corona, wakulima wanasema hawahisi kauli hiyo.

“Bado tungali kwenye mataa. Ni muhimu serikali itangamane na wakulima nyanjani,” Njoki ahimiza.

Mkulima huyu hata hivyo anasisitiza hayupo radhi kuasi kilimo cha ndizi, akisema changamoto anazopitia ni za muda tu.

Kwa kuzingatia taratibu faafu kitaalamu, ekari moja ina uwezo kusitiri kati ya migomba 450 – 550.

“Upanzi, nafasi ya mita 2.5 hadi 5 kati ya miche ya migomba ndiyo bora,” ashauri Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya matunda na miti, na kuongeza kuwa mbolea ya mifugo ndiyo faafu na ichanganywe na udongo na fatalaiza.

“Kilimo cha matunda kinafanikishwa na uwepo wa maji ya kutosha,” asisitiza, akielezea haja ya kukumbatia mfumo wa mifereji kunyunyizia mimea na mashamba maji.

“Mataifa kama vile Misri na Israili, yameibuka kuwa bora katika uzalishaji wa matunda kwa sababu ya mfumo wa kuvuna maji licha ya kuwa jangwa. Kenya tuna hali bora ya anga na maji ya kutosha, muhimu ni kuweka mikakati kabambe kuyavuna ili kufanya kilimo,” Mwenda anafafanua.

Hannah Njoki anasema hutegemea maji ya mvua, ombi lake kwa serikali ya Kaunti ya Kiambu na pia ya kitaifa likiwa kuzindua miradi ya maji ili aendeleze azma yake katika ukuzaji wa ndizi.

Mwanazaraa huyu anaendelea kutathmini suala la uongezaji mazao yake thamani, hasa kuyaivisha ili kuwahi soko bora.

Mbali na ukuzaji wa ndizi, Njoki pia ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi na kuku, mbolea ya mifugo hao akiitumia kuboresha migomba.

You can share this post!

AKILIMALI: Mkulima anavyochuma kutokana na matundadamu

AKILIMALI: Anafuma mavazi maridadi kutumia nyuzi za krocheti