Demu avamia polo kwa kutomtongoza

Na JOHN MUSYOKI

MAKONGENI, THIKA

KIDOSHO mmoja mtaani hapa alimzaba kofi jamaa mmoja kwa kukataa kumtongoza.

Demu alikuwa na mazoea ya kumtembelea jamaa huyo katika chumba chake cha kupangisha kwa nia ya kujipendekeza ili atongozwe.

Hata hivyo, mpango wa mwanadada huyo uligonga mwamba jamaa alipompuuza kwa sababu alikuwa akijua tabia yake ya kunyemelea wanaume.

“Demu alikuwa na tabia ya kuwanyemelea wanaume na wakishaonja tunda, anawatapeli na kutoroka,” alisema mdokezi.

Inasemekana licha ya kumtembelea jamaa huyo mara kadhaa, hakufaulu kumuingiza kwa boksi.

Siku ya kioja, demu alikosa subira na kuamua kumgutusha jamaa kwa kumzomea vikali kisha akamzaba makofi.

“Kwani wewe ni mwanamume sampuli gani? Tangu nilipoanza kukutembelea hujawahi kung’amua kwamba ninakupenda? Ni mistari umekosa au huna hisia?” demu alimkaripia polo.

Jamaa kwa upande wake alimweleza demu kwamba hakuwa na haja naye.

“Nilijua kwamba unajipendekeza kwangu. Sina shughuli na wewe. Kaa tu ule na utazame runinga na ukichoka urudi kwako. Umekuwa na wanaume chungu nzima na mnaachana kwa sababu ya ujeuri wako. Usidhani mimi ni fala nikurukie haraka hivyo. Tafadhali bahatisha kwa mtu mwingine lakini kwangu, sahau,” jamaa alisema.

Inasemekana hata kabla ya jamaa kumaliza kauli yake, demu alimzomea kisha akamzaba kofi. “Ninyamazie gumegume wewe. Sijawahi kuona mtu mwoga kama wewe. Mwanamume ni kuramba asali. Lakini sitakulaumu sana, labda jembe lako haliwezi kulima shamba vizuri,” demu alimwambia jamaa.

Jamaa alihisi uchungu ila hakulipiza kisasi kwa kuwa aliamini alikuwa amemzidi demu huyo maarifa naye demu akaondoka na hakurudi kwake tena.