• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
WASONGA: Knut, Kuppet zisitishe migomo wakati huu

WASONGA: Knut, Kuppet zisitishe migomo wakati huu

Na CHARLES WASONGA

TISHIO la walimu kwamba watagoma endapo Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) haitawaongezea mishahara na marupurupu, halifai kwani hiyo itavuruga zaidi kalenda ya masomo ambayo tayari ilifanyiwa mabadiliko kufuatia janga la Covid-19.

Pili, uchumi wa nchi umelemazwa pakubwa na janga hilo na kuchangia TSC, kwa ushauri wa Wizara ya Fedha, kusitisha nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma kwa kipindi cha miaka miwili ijayo.

Vile vile, ni unafiki kwa uongozi mpya wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) kutisha kuitisha mgomo ilhali wiki jana uliahidi kushirikiana na TSC kuleta utulivu katika sekta ya elimu.

Kwenye kikao na wanahabari dakika chache baada ya kuchaguliwa bila kupigwa, Katibu Mkuu mpya Collins Oyuu alisema chini ya hatamu yake atakumbatia moyo wa mazungunzo katika kutetea masilahi ya walimu badala ya makabiliano, alivyofanya mtangulizi wake, Wilson Sossion.

Ama kwa hakika, alijitokeza kama kiongozi mnyenyekevu ambaye anapania kujijengea sifa ya kipekee kama mpatanishi wala sio mpenda makabiliano.

Lakini kinaya ni kwamba sasa baada ya kufanya kikao cha kwanza na TSC, Bw Oyuu amebadilika na kuungana na mwenzake wa KUPPET, Akelo Misori kutoa ilani kwa TSC kwamba walimu watagoma kuanzia Julai 26 shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Wakenya, na hata walimu, wenyewe wanafahamu fika kuwa utepetevu wa viongozi wa Knut na Kuppet ndio umechangia vyama hivyo kuisha nguvu za kutetea masilahi ya wanachama wao.

Itakumbukwa kwamba wakati wa hatamu ya Bw Sossion, kama Katibu Mkuu wa Knut, Bw Misori na wenzake wa Kuppet waliruhusu TSC kuwagawanya.

Kwa mfano, mwaka 2019 TSC iliwapa wanachama cha Kuppet nyongeza ya mishahara na marupurupu chini ya mkataba (CBA) ya 2016 -2021 na kuwaza wanachama wa Knut.

Sababu kuu ilikuwa kwamba uhusiano kati ya TSC na Knut haukuwa mzuri wakati huo, hali iliyochangia tume hiyo kuondoa jina la Bw Sossion kwenye orodha ya walimu inayowatambua.

Vile vile, ni wakati huo ambapo TSC ilizima utaratibu wa zamani ambapo ilikuwa ikikata na kuwasilisha michango ya wanachama wa KNUT kwa akaunti ya chama hicho. Hatua hiyo imefilisha Knut kiasi cha kushindwa kulipa kodi ya afisi zake katika kaunti mbalimbali, kulipa mishahara ya wafanyakazi na kugharamia shughuli zake zingine.

Hatua hiyo, bila shaka, ilisababisha walimu wengi kugura Knut na kujiunga na Kuppet. Hii ndio maana idadi ya wanachama wa Knut ilipungua kutoka zaidi ya 200,000 hadi wanachama 17,000 sasa.

Kwa hivyo, ni makosa kwa Mbw Misori na Oyuu sasa kutisha TSC kwamba wataisha mgomo ilhali wao ndio waliruhusu TSC na Serikali kuwagawanya na hivyo kudhoofisha nguvu zao za kutetea masilahi yao.

Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu. Utangano wa Knut na Kuppet ndio umeruhusu serikali na TSC kufanikisha mpango wa kuvilemaza na hivyo kukosa nguvu ya kutetea masilahi ya wanachama wao.

Kwa hivyo, Mbw Oyuu na Misori walijipige vifuo kwamba watavurugu shughuli za masomo na hivyo kuathiri wanafunzi na wazazi ilhali shimo ambalo wamejipata kwalo ni wao walijimbia wenyewe.

You can share this post!

Uhuru afinya raia usiku

Waliofungwa jela maisha kwa kuficha gaidi wa al-Qaeda...