• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Familia 50 zaumizwa na baridi kali baada ya nyumba zao kuteketea Mukuru-Kayaba

Familia 50 zaumizwa na baridi kali baada ya nyumba zao kuteketea Mukuru-Kayaba

Na SAMMY KIMATU

FAMILIA 50 zilikesha nje penye baridi baada ya nyumba zao kuteketea kwenye mkasa wa moto usiku wa kuamkia Jumapili.

Kisa hicho kilitokea katika eneo la Budalangi lililoko katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, kaunti ndogo ya Starehe.

Maafisa wa kuzima moto walikosa barabara ya kuingia kwenye eneo la mkasa kutokana na msongamano wa nyumba.

Licha ya hayo,ililazimu magari mawili ya kuzima moto kutoka kwa serikali ya kaunti ya Nairobi kuzunguka na kuingia ndani ya kituo cha umeme cha kampuni ya Kenya Power mkabala wa barabara ya Enterprise.

Ili kuzuia waporaji, maafisa wa polisi wakiongozwa na kamanda wa eneo la South B, Bw Samuel Ochoki walihakikisha usalama umedumishwa.

Mwathiriwa mmoja aliye kadhalika mmiliki wa nyumba nne, Bi Faith Musivulu, 35, aliyeishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitano alisema moto ulianzia ndani ya nyumba moja ambapo mwenyewe alikuwa amelala.

Majirani waliongeza kwamba mama wa watoto watano aliyedaiwa kuwa mlevi alisahau kuzima mshumaa kabla ya kulala fofofo.

Kwa bahati nzuri, watoto wote watano walikuwa wameenda kupata chakula cha jioni kwa nyumba tofauti ambako babake huishi.

“Mwanamke alikuwa amewasha mshumaa na kulala kabla ya kuuzima. Akiwa usingizini, mshumaa uliwakisha pazia ya nyumba kabla ya nyumba yote kuwaka na kusambaa kwa nyumba jirani,” Bi Faith akasema.

Ni wakati ambapo jirani yake alipoona neti yake imewaka moto aliamsha mkewe na mara moja kuchukua mtoto wao wa miaka mitatu na kutoroka.

Familia hiyo iliondoka bila chochote huku mali yote yao ikiteketea na kubakia kuwa majivu.

Mwathiriwa mwingine, Bi Sabina Wamaitha, 38 alisema licha ya maji kukosekana mtaani, vijana walishirikiana kubomoa nyumba huku wengine wakipanga foleni hadi ndani ya mto Ngong.

“Vijana walibomoa nyumba ili kuzuia moto kuenea zaidi na wengine wao wakitumia maji ya mto Ngong kuuzima kwani maji ya mifereji yanayosambazwa mtaani kwa mgao na kampuni ya Nairobi Water hufungwa leo,” Bi Wamaitha akasema.

Viongozi wa vijana katika eneo hilo, Bw Benson Kivindu Kilonzi aka Bentos na Bonface Ogutu Jubilee walisema kufuatia msururu wa visa vya moto mtaani huo kwa miaka ya hapo nyuma, vijana hushirikiana vizuri wakati wa majanga.

“Nawapongeza vijana wangu kwa kujitoa kwa moyo mara kunapokuwa na visa vya moto na wakati kuna mafuriko mtaani wetu,” Bw Bentos akasema.

Tukienda mitamboni, mwakilishi wa wodi, Bw Herman Azangu aliahidi kuwatembelea waathiriwa na kutoa msaada wake kutoka kwa serikali ya kaunti.

You can share this post!

Corona hatari sana yaja hata kwa waliopata chanjo –...

Patrick Vieira apokezwa mikoba ya ukocha kambini mwa...