• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Usimpake tope Raila, wabunge wa ODM wamuonya Ruto

Usimpake tope Raila, wabunge wa ODM wamuonya Ruto

Na DAVID MWERE

WABUNGE wandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga Jumatatu jioni walimkaripia Naibu Rais William Ruto, wakimtaka kukoma kumtaja kiongozi huyo wa upinzani katika sakata za ufisadi.

Bw Moitalel Ole Kenta (Narok Kaskazini), Anthony Oluoch (Mathare), Caleb Amisi (Saboti) na Mbunge Maalum wa ANC Godfrey Osotsi walidai Bw Odinga ni “safi” na kwamba ni Dkt Ruto ambaye amewahi kutajwa katika sakata kadha za ufisadi.

“Wakati masuala ya ufisadi yanapotajwa, yeye hujitokeza na kujitetea. Anamaanisha kwamba yeye na ufisadi ni kitu kimoja,” Bw Oluoch akauliza.

“Tunashangaa kwamba Dkt Ruto anamhusisha Bw Odinga na ufisadi ilhali huyo ni kiongozi ambaye hayuko serikalini. Wandani wake Dkt Ruto ndio wamefunguliwa mashtaka ya ufisadi mahakamani,” Bw Kenta akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Mbona analalamika ilhali Bw Odinga hakutaja jina la mtu yeyote alipozungumzia kuhusu kero hili alipokuwa kule Mombasa? Mbona anadhani ni yeye aliyerejelewa?” akauliza Bw Amisi.

Wakati wa ziara yake katika eneo la Pwani mwishoni mwa wiki, Bw Odinga, bila kutaja jina la mtu yeyote, alisema atawasukuma gerezani viongozi wote wafisadi ikiwa atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao.

Lakini akiongea baada ya kuhudhuria Ibada ya Jumapili katika eneo bunge la Embakasi Magharibi, Nairobi Dkt Ruto ambaye pia anakimezea mate kiti cha urais 2022, alimhusisha Bw Odinga na sakata ya ufisadi ya mpango wa Kazi kwa Vijana, alipohudumu kama Waziri Mkuu wakati wa serikali ya muungano mkuu.

Vile vile, Naibu Rais alidai kuwa Odinga na washirika wake walihusika katika sakata ya kima cha Sh7.6 bilioni ya ununuzi wa dawa katika mamlaka ya ununuzi wa dawa nchini (KEMSA).

Lakini Jumatatu wabunge hao wakereketwa wa chama cha ODM walimwondolea Odinga lawama na kusema kuwa Dkt Ruto ambaye yuko serikalini ndiye anapaswa kulaumiwa kwa sakata hiyo ya Kemsa, almaarufu “ Covid Billionaires”

Vile vile, Bw Ole Kenta, Oluoch, Amisi na Osotsi walimlaani Bw Odinga kutokana na mwenendo wake wa kudai kila mara kwamba alimsaidia Rais Uhuru Kenyatta kupata wadhifa huo katika chaguzi za 2013 na 2017.

Dkt Ruto pia amekuwa akidai kuwa ni kutokana na juhudi zake ambapo Bw Odinga aliweza kupata kiti cha Waziri Mkuu wakati wa utawala wa Serikali ya Muungano Mkuu mnamo 2008.

“Kila Mkenya anajua kwamba Bw Odinga alipata wadhifa wa Waziri Mkuu kupitia mchakato wa maridhiano ambayo yaliongozwa na Umoja wa Afrika (AU). Kwa hivyo, Dkt Ruto asiwahadae Wakenya kwamba yeye ndiye aliyemsadia Odinga kupata cheo hicho,” akasema Bw Oluoch ambaye ni wakili.

Bw Osotsi pia alimsuta Dkt Ruto kwa kudai kuwa serikali ya Rais Kenyatta imefeli kutimiza ahadi zake kwa raia katika kipindi chake cha pili cha mamlakani.

“Ikiwa Rais amefeli, basi yeye kama Naibu Rais pia amefeli. Hawezi kujitenga na kufeli huko kwa sababu wote wawili walichaguliwa kwa tiketi moja. Ruto akome kuwahadaa Wakenya kupitia propaganda zisizo na msingi wowote,” akasema Bw Osotsi.

Tangu Rais Kenyatta aliridhiane kisiasa na Bw Odinga kupitia kwa kusalimiana nje ya Jumba la Harambee mnamo Machi 18, 2018, Naibu Raia amekuwa akijifanya kama mwanasiasa wa upinzani huku akishambulia serikali. Hii ni licha ya kudinda kujiuzulu na amekuwa akiendelea kufurahia mamlaka ya afisi ya Naibu Rais.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Wawindaji haramu watupwa jela miaka 16

Wanachama 500 wagura UDA na kurejea ODM