• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Tanzania mbioni kuunda chanjo yake ya corona

Tanzania mbioni kuunda chanjo yake ya corona

Na MWANDISHI WETU

TANZANIA imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya virusi vya corona ili kupunguza gharama ya kuiagiza kutoka nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema kuwa chanjo hiyo itatengenezewa kwenye kiwanda ambacho kimeanza kujengwa.

Alisema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama ya kuiagiza kutoka nje ya nchi na pia kuileta karibu na wananchi.

Prof Makubi alisema mpango huo wa kutengeneza chanjo umeidhinishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katibu huyo, hata hivyo, hakuelezea hatua ambayo kiwanda hicho kinachojengwa kimefikia.Prof Makubi pia hakuelezea ni lini chanjo ya corona itaanza kutengenezewa nchini Tanzania.

Mataifa mengine ambayo yametangaza mpango wa kujitengenezea chanjo barani Afrika ni Afrika Kusini, Uganda, Senegal na Rwanda.

Hakuna nchi ya Afrika ambayo imeanza kujitengenezea chanjo kufikia sasa.Prof Makubi alisema serikali ilichukua uamuzi huo kwa sababu ina wataalamu waliobobea katika utengezaji wa chanjo.

“Tuna wataalamu waliohitimu kwa hivyo tunataka huo mchakato wa kuanza kutengeneza chanjo zetu humu nchini. Vilevile, tutatengeneza chanjo za maradhi mengine mbali na corona,” akasema Prof Makubi alipokuwa akizungumza Jumapili jijini Dodoma.

Prof Makubi pia alitangaza masharti mapya yanayolenga kuzuia kusambaa kwa corona shuleni na vyuoni.

Kuanzia jana, walimu, wanafunzi na wafanyakazi wote walitakiwa kuvalia barakoa wakati wote wanapokuwa shuleni au vyuoni.

Wanafunzi watavalia barakoa hata watakapokuwa darasani.Vifaa vya kunawa mikono na kutupa taka pia vitaweka nje ya vyumba vya madarasa na mabweni.

Wanafunzi pia watatakiwa kupewa mafunzo kuhusu ugonjwa wa corona na jinsi ya kujilinda dhidi ya maambukizi.

Wanafunzi watakaoshukiwa kuwa na virusi vya corona watapelekwa katika hospitali iliyo karibu ili wapewe huduma ya haraka.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Rais Suluhu, nchi hiyo ya Afrika Mashariki ina wagonjwa 100 wa corona na kati yao 70 wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi na wamewekewa hewa ya oksijeni.

Tanzania tayari imetuma maombi ya kutaka kujiunga na mpango wa Covax ambao husaidia mataifa maskini, haswa barani Afrika, kupata chanjo nafuu.

Chanjo kupitia mpango wa Covax inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kati ya Desemba, mwaka huu, na Januari mwaka ujao, kwa mujibu wa Prof Makubi.Katibu wa wizara alisema kuwa chanjo ya corona itatolewa kwa wananchi bila malipo.

“Serikali haitaruhusu wafanyabiashara wa kibinafsi kuingiza chanjo ya corona humu nchini bila kufuata utaratibu utakaowekwa,” akasema.

You can share this post!

Nani safi kati ya Raila na Ruto?

Tofauti zaibuka kuhusu uteuzi Kadhi wa kike