• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Matiang’i aahidi kukomesha utekaji nyara nchini

Matiang’i aahidi kukomesha utekaji nyara nchini

Na NDUNGI MAINGI

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ameahidi kukabiliana na visa vya utekaji nyara ambavyo vimeongezeka nchini.

Akihutubia maafisa wakuu wa usalama katika Chuo cha Mafunzo ya Serikali (KSG) jijini Nairobi, Dkt Matiang’i alisema serikali ina habari kwamba baadhi ya visa hivi vinatokana na biashara haramu zinazoendeshwa kichinichini.

“Tuna habari baadhi ya visa vya utekaji nyara nchini vinatokana na biashara haramu na tuko mbioni kukabiliana navyo,” alisema.

Waziri huyo alisema kwamba visa hivyo ambavyo vimezua hofu nchini ni suala dogo kwa idara ya usalama na vitakomeshwa.

Alipendekeza maafisa wa usalama wabuni mbinu mpya za kukabiliana na visa vya uhalifu nchini na kuwahimiza kuhusisha raia na hasa viongozi wa kidini.

Mkutano huo uliowaleta pamoja wakuu wa usalama wa kaunti zote, ulijadili jinsi ya kudumisha usalama hasa wakati huu nchi inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Kuhusu visa vya masuala yanayoathiri maafisa wa usalama, Dkt Matiang’i aliahidi kuhakikisha malalamishi yao yanashughulikiwa.

Baadhi ya maafisa wa usalama wa vyeo vya chini wamekuwa wakitumia mitandao ya kijami kutoa malalamishi yao.

Dkt Matiang’i alisema madai yote yatachunguzwa ili ukweli ubainike.Vilevile aliahidi kuimarisha maadili miongoni mwa maafisa wa usalama na kuwachukulia hatua wale wanaokiuka haki za wananchi.

“Nina habari kuhusu yaliyotukia Kisii na uchunguzi unaendelea ili kuwachukulia hatua wahusika,” alisema.

Kumekuwa na visa vya maafisa wa usalama kuua raia katika kaunti hiyo. Katika kisa kimoja, mshukiwa alifariki katika hali ya kutatanisha akizuiliwa seli za polisi na mwingine akadaiwa kupigwa risasi kimakosa na maafisa wa usalama.

Waziri aliwashukuru wakuu wa polisi kote nchini kwa kukabiliana na makosa madogo madogo.

Wakati huo huo Dkt Matiangi aliwahakikisha Wakenya usalama utadumishwa kabla na kwenye uchaguzi mkuu ujao huku akionya wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi ya chuki na uchochezi.

“Msitiwe hofu yoyote. Msitilie maanani maneno ya wanasiasa wasio na maono ambao nia yao ni kuvuruga utulivu,” alisema Matiang’i.Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai na Katibu wa Wizara ya Usalama wa ndani Karanja Kibicho walihudhuria mkutano huo.

You can share this post!

Wabunge watisha kumtimua Magoha

Mchakato kusaka Naibu Gavana wa Nairobi waanza