• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Aliyekuwa mchezaji wa Harambee Stars aendelea kutatizika nyumbani

Aliyekuwa mchezaji wa Harambee Stars aendelea kutatizika nyumbani

NA ABDULRAHMAN SHERIFF 

ALIYEKUWA mchezaji wa Harambee Stars na klabu kadhaa maarufu za hapa nchini, Abdalla Juma anaendelea kutatizika na msongo wa mawazo (depression) uliompelekea kutocheza soka la hali ya juu.

Juma aliyewahi kuzichezea klabu za Thika United, Sofapaka, AFC Leopards na Posta Rangers FC amekuwa na tatizo hilo la msongo wa mawazo kwa miaka kadhaa ambapo amekuwa hachezi tena klabu kubwa.

Mamake Amina Hussein anasema Juma alipogundulika kuwa na tatizo hilo, waliokuwa waajiri wake (jina twalibana) pamoja na maafisa wa mpira wa miguu hawakujitokeza kumsaidia kwa njia yoyote.

“Juma yuko nyumbani akiishi bila kazi na hakuna mchezaji wa klabu alizochezea au aliocheza nao timu ya taifa aliyewahi kumtembelea,” alisema Amina.

Taifa Leo ilipomtembelea nyumbani kwa jamaa yake Utange, karibu na Kituo cha Wema kaunti ndogo ya Kisauni, Juma hakuweza kujibu maswali aliyoulizwa kutokana na ilivyo hali yake.

“Bado nipo uwanjani, nafanya mazoezi na najiandaa kurudi kucheza timu ya taifa. Shida yangu sina kazi na ninataka kucheza mpira,” hayo ndiyo maneno ya pekee Juma aliweza kuyatamka kwenye mahojiano.

Mama yake alisema Juma huwa hajishughulishi na mazungumzo yoyote mbali na soka. “Neno mpira wa miguu ndio kitu ambacho anakitaja zaidi kinywani mwake,” alisema Amina.

“Juma ana hamu ya kuchezea timu yoyote kubwa na pia timu ya taifa. Hatuwezi kumsaidia lakini tuna hakika kwa msaada kutoka kwa wakuu wa michezo, ataweza kushinda tatizo hilo,” alisema. .

Amina anasema hali ya mtoto wake inaweza kuboreshwa haraka ikiwa atawekwa chini ya uangalizi wa mtu. “Tunaishi naye lakini ingekuwa bora ikiwa anaweza kuwekwa chini ya mlezi,” alisema.

Ametoa wito kwa wachezaji waliocheza na mwanawe na maafisa wa michezo kuwatembelea kujionea hali ya Juma. “Nina imani mwanangu akipata matibabu anayostahili, anaweza kurudi kucheza tena,” akasema.

Licha ya hali yake, Juma huwa anafanya mazoezi na timu ya mtaani ya Bilima FC.

You can share this post!

Serikali yatoa Sh8.7 bilioni kusaidia familia maskini

TANZIA: Hillary Ng’weno afariki, aacha historia ya...