• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
CHARLES WASONGA: Ni mapema kwa viongozi kuhama vyama, kubuni miungano

CHARLES WASONGA: Ni mapema kwa viongozi kuhama vyama, kubuni miungano

Na CHARLES WASONGA

S IASA ni telezi na hubadilika kila dakika. Hii ndio maana wajuzi wa masuala haya husema hivi: “Siku moja katika siasa ni sawa na mwaka mmoja katika hali halisi”.

Ni kwa misingi hii ambapo nahisi kwamba ni mapema sana kwa wanasiasa kutangaza misimamo yao ya kisiasa kuhusiana na uchaguzi mkuu ujao, utakaofanyika miezi 13 ijayo.

Vile vile, ni mapema mno kwa vyama vya kisiasa kuanza mipango ya kubuni miungano kwa lengo la kushinda katika uchaguzi huo.

Mabadiliko yanaweza kutokea katika uwanja wa siasa na wanasiasa ambao tayari wamehamia vyama vingine wakajipata wakitamani kurejea katika vyama vyao vya awali.

Aidha, miungano inayobuniwa wakati kama huu huenda ikakumbwa na misukosuko, mivutano na kutoelewana miongoni mwa wanasiasa washirika na hivyo kusambaratika hata kabla ya siku ya uchaguzi; Agosti 9, 2022.

Kwa mfano, juzi Mbunge Mwakilishi wa Kiambu Gathoni Wamuchomba alitangaza kuwa amegura mrengo wa Kieleweke, katika chama cha Jubilee, chake Rais Uhuru Kenyatta na kujiunga na ule wa Tangatanga unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Hii ilimaanisha kuwa, kimsingi, Bi Wamuchomba ameasi chama cha Jubilee na kuhamisha uaminifu wake kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Dkt Ruto.

Mbunge huyo alisema alichukua hatua hiyo kutokana na kile alichokitaja kama “udikteta” ndani ya Jubilee.Vile vile, alisema alichukua hatua hiyo kutokana na mchango wa chama hicho kubuni muungano na ODM “bila kutushauri sisi kama wanachama”.

Kwa mtazamo wangu, sababu hizi hazina mashiko hata chembe. Sababu kuu iliyochangia mwanasiasa huyu, na wenzake wengine kutoka Mlima Kenya, kuhamia kambi ya Dkt Ruto ni dhana kwamba naibu huyo wa rais ni maarufu miongoni mwa raia wa eneo hilo.

Hii ni kutokana na kile kinachoaminika kama hatua ya Rais Kenyatta kuwasaliti kisiasa kwa kuridhiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia handisheki.

Inakisiwa kuwa Rais Kenyatta ataunga mkono azma ya Bw Odinga kuingia Ikulu kinyume na ahadi yake ya awali kwamba angemuunga mkono Dkt Ruto.

Swali langu ni je, wanasiasa hawa watachukua hatua gani endapo handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga itaporomoka kiongozi wa taifa atakapoamua kumuunga mkono mgombeaji mwingine?

Tasnifu yangu ni kwamba hilo linawezekana kwani tayari Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amejitosa katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Alitoa tangazo hilo siku chache tu baada yake kutawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya, hatua ambayo inaaminika kuungwa mkono na Rais Kenyatta.

Kwa upande mwingine, mipango ya vyama vya Jubilee na ODM kubuni muungano kwa ajili ya kuimarisha nafasi yao ya kushinda katika uchaguzi mkuu wa 2022, tayari imeanza kukumbwa na sintofahamu.

Hii ni baada ya baadhi ya wanachama wa Jubilee kushikilia kuwa wanaweza tu kubuni muungano na NASA (inajumuisha vyama vya Wiper, ANC na Ford Kenya) wala sio ODM.

Ndiposa nasisitiza kuwa ni mapema kwa wanasiasa kuanza kuhamia vyama vingine au vyama kubuni miungano kwa sababu uwanja wa siasa ni telezi na unaweza kubadilika kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2021.

Wakati mwafaka ni kuanzia Februari mwaka ujao, wakati ambapo watumishi wa umma wanaotaka kuwania nyadhifa uchaguzini watahitajika kujiuzulu.

You can share this post!

Avutiwa kwa filamu na kipindi cha ‘Pete’

BENSON MATHEKA: Ripoti ya Kriegler itekelezwe kusaidia...