• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
BENSON MATHEKA: Ripoti ya Kriegler itekelezwe kusaidia polisi humu nchini

BENSON MATHEKA: Ripoti ya Kriegler itekelezwe kusaidia polisi humu nchini

Na BENSON MATHEKA

VISA vya maafisa wa polisi kuua wenzao, kujiua na kuua familia zao vinaonyesha kwamba kuna tatizo kubwa ndani ya kikosi hicho ambalo limepuuzwa kwa miaka mingi.

Tatizo hilo linatokana na kutotekelezwa kwa mageuzi yaliyopendekezwa na tume iliyoongozwa na Jaji Mstaafu wa Afrika Kusini Joan Kriglier.

Tume hiyo ilipendekeza kuwa kikosi cha polisi kibadilishwe kuwa huduma ya polisi ili kupalilia utaalamu miongoni mwa maafisa wa polisi.

Mageuzi hayo yangewafanya maafisa hao kuheshimu haki za binadamu, kubuniwa kwa vitengo mbali mbali kama vile vya kuwapa ushauri nasaha, kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo kukataa amri iliyo kinyume cha sheria au inayokiuka haki za binadamu kutoka kwa wakubwa wao miongoni mwa mageuzi mengine.

Kulingana na ripoti ya Kriglier, mageuzi hayo yangewafanya maafisa wa polisi kutekeleza kazi yao ya utumishi kwa wote kwa utaalamu huku wakiwajibika kwa katiba pekee na sheria za nchi.

Hata hivyo, mageuzi yaliyoanza kutekelezwa chini ya katiba mpya ya 2010 yalilemazwa na serikali iliyotaka kuwatumia kwa manufaa ya kulinda maslahi ya walio mamlakani na kusahau maslahi ya maafisa wa polisi.

Japo jina lilibadilishwa hadi Huduma ya Taifa ya Polisi, ni wazi kuwa hii ilifanyika kwa maandishi pekee. Kwa mfano, serikali ilipokonya Tume ya Huduma ya Taifa ya Polisi uhuru wake wa kuteua Inspekta Jenerali wa polisi na kurejesha mtindo wa zamani wa maafisa wa polisi kuwajibika kwa walio mamlakani badala ya katiba na sheria za nchi.

Serikali ilifuta pendekezo kwamba maafisa wa polisi wawe na alama ya C katika mtihani wa kidato cha nne ikaanza kuajiri waliopata alama ya D.

Maslahi ya maafisa wa polisi yalitupwa kwenye kaburi la sahau wakatelekezwa licha ya mazingira magumu ya kazi yanayoathiri afya yao kiakili. Hii pamoja na amri za kiimla na dhuluma kutoka kwa baadhi ya wakubwa wao zimewazidishia matatizo ya akili.

Licha ya baadhi yao kutumia mitandao ya kijamii kulalamikia dhuluma wanazotendewa na kupuuzwa kwa maslahi yao, walichofanya wakubwa wao ni kutisha kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Kinachohitajika kuepusha maafisa wa polisi na matatizo ya akili ni kuimarisha mazingira yao ya kazi kwa kutekeleza kikamilifu mageuzi yaliyopendekezwa katika ripoti ya Kriglier. Kutumia njia za mkato hakutaleta suluhu ya kudumu.

Maafisa hao ni binadamu na haki zao zinafaa kulindwa. Hawafai kutumiwa kama vifaa vya kutimiza maslahi ya wakuu wao na walio mamlakani.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ni mapema kwa viongozi kuhama vyama,...

Museveni ataka nchi zote za Afrika zitumie Kiswahili