• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
WARUI: Nafasi 10,000 za kazi TSC ilitangaza ni chache mno

WARUI: Nafasi 10,000 za kazi TSC ilitangaza ni chache mno

Na WANTO WARUI

KATIKA jaribio la kuziba pengo la ukosefu wa walimu nchini, Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini, TSC imetangaza nafasi za kazi kwa walimu wapatao 10,000 ambao wanatarajiwa kuhojiwa kati ya Julai na Agosti 2021 kabla ya kuajiriwa.

Katika idadi hii, walimu wapya wapatao 4,000 wanatarajiwa kujiunga na shule za sekondari, 927 kuziba pengo la walioondoka 1,000 wa shule za msingi wapandishwe vyeo, walimu wengine wapya 1,000 waajiriwe kufunza shule za msingi nao walimu 2,987 kuziba pengo la walimu walioondoka katika shule za msingi.

Kwa mtazamo huu, idadi ya walimu wanaoajiriwa ni ndogo mno ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi ambao wanatarajiwa kuhudumiwa na walimu hao.

Shule za sekondari zinatarajia kupokea idadi kubwa zaidi ya wanafunzi kutokana na mpango wa serikali wa kuhakikisha kila mwanafunzi aliyefanya mtihani wa KCPE amejiunga na shule ya sekondari.

Ili kuweza kukabiliana na hali hii, ni lazima walimu wa kutosha wawepo katika shule hizo. Aidha, shule za msingi nazo zinaendelea kupokea wanafunzi wengi zaidi kadri siku zinavyopita. Idadi ya walimu wapya wanaoajiriwa katika shule hizi za msingi hailingani kamwe na mahitaji ya wanafunzi.

Vilevile TSC inachukua muda mrefu kujaza pengo la walimu wanaostaafu, kufariki ama kuacha kazi kwa sababu nyinginezo na inapoamua kufanya hivyo, haiajiri idadi sawa ya walimu na ile iliyoondoka. Hili linasababisha uhaba wa walimu shuleni hivyo basi kutatiza utoaji wa elimu bora.

Kuna uhaba wa walimu wengi kote nchini. Katika shule nyingi za umma hasa zile za msingi, mwalimu hulazimika kusimamia zaidi ya wanafunzi sitini au zaidi.

Madarasa yamefurika wanafunzi ambao wengine wanaishi na vitabu ambavyo havijasahihishwa na mwalimu. Kipindi cha mafunzo cha dakika 35 ambapo mwalimu hutarajiwa afunze, wanafunzi wafanye kazi na mwalimu asahihishe kazi hiyo kinakuwa tu ni cha desturi kwa kuwa mwalimu hawezi kusahihisha kazi za wanafunzi wote kwa muda huo, hivyo basi inakuwa vigumu kutambua wale ambao hawakuelewa.

Hii ndiyo sababu wazazi wengi wenye kipato ingawa kidogo wanakimbilia shule za kibinafsi ambako wanahisi kuna walimu wa kutosha na idadi ya wanafunzi kwa kila mwalimu haipiti 25.

Hii ni changamoto kubwa kwa serikali na itahitaji kujifunga kibwebwe ili kukabiliana na shida hii. Kwa sasa, idadi ya walimu wanaoajiriwa na TSC ni nzuri ila bado ni ya chini mno. Huku uajiri huo ukiendelea, pana haja pawe na uwazi na uwajibikaji katika shughuli hii yote.

You can share this post!

TAHARIRI: Elimu si jukumu la serikali pekee

WASONGA: Mashirika ambayo ni zigo kwa mlipa kodi yafungwe