• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
WASONGA: Mashirika ambayo ni zigo kwa mlipa kodi yafungwe

WASONGA: Mashirika ambayo ni zigo kwa mlipa kodi yafungwe

Na CHARLES WASONGA

TANGAZO la Wizara ya Fedha kwamba, imeanzisha hatua za kupunguza idadi ya mashirika ya serikali ili kudhibiti gharama kwa serikali limesheheni busara tele.

Japo hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali kutimiza masharti iliyowekewa na Shirika la Kifedha Ulimwenguni (IMF) lilipoipa mkopo wa Sh255 bilioni, itaokoa fedha nyingi zinazoweza kuelekezwa kwa maendeleo.

Chini ya mpango huo, uliotangazwa Alhamisi na Waziri wa Fedha Ukur Yatani, serikali inapania kubinafsisha na kubadili usimamizi wa jumla ya mashirika yake 18.

Mashirika hayo kama Kenya Airways yamekuwa yakiandikisha hasara kila mwaka, hali ambayo hulazimisha serikali kuyanusuru kwa kuyapatia pesa zaidi. Isitoshe, mashirika haya yamezongwa na mzigo mkubwa wa madeni ambayo yameshindwa kulipa.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Fedha, inakadiriwa kuwa mashirika hayo ya serikali yanadai karibu Sh170 bilioni, ambazo ni malimbikizi ya mikopo iliyodhaminiwa na serikali kuu.

Tayari, ripoti ya ukaguzi imefichua kuwa, serikali inahitaji Sh70 bilioni kila mwaka kufadhili shughuli za mashirika hayo, miongoni mwao ikiwa ni shirika la usambazaji umeme nchini (Kenya Power), Shirika la Reli Nchini (Kenya), Vyuo Vikuu vya Nairobi (UoN), Kenyatta na Moi, miongoni mwa taasisi zingine. Utekelezwaji wa mageuzi ya usimamizi, sawa na yaliyotangazwa katika UoN juzi na ubinafsishwa wa mashirika hayo bila shaka itaokoa mlipa ushuru pesa hizi (Sh70 bilioni) na kuzuia ongezeko la mzigo wa deni.

Japo mpango huu utapelekea idadi kubwa ya wafanyakazi kupoteza ajira, unafaa kabisa haswa nyakati kama hizi ambapo uchumi wa Kenya na ulimwengu kwa ujumla umeathiriwa na makali ya janga la Covid-19.

Vile vile, mageuzi kama hayo yataiwezesha serikali kupunguza kiwango chake cha madeni ambacho sasa kinaelekea kufikia kima cha Sh9 trilioni.

Zoezi la ukaguzi wa mashirika ya serikali yasikomee 18 ambayo yamependekezwa kufanyiwa mageuzi, bali lihusishe pia mashirika mengine ambayo hayana faida. Kwa kufanya hivyo, huenda ikabainika kuna mashirika mengine zaidi yanazongwa na changamoto sawa na yale yaliyogunduliwa katika 18 yanayolengwa sasa.

Haina maana kwa serikali ya Kenya kuendelea kufadhili zaidi ya mashirika 200 ya umma ambayo hayaleti manufaa yoyote kwa uchumi wa nchi.

Itakumbukwa kwamba mnamo 2015, miaka mitatu baada ya serikali ya Jubilee kuingia mamlakani, Rais Kenyatta aliteua jopo kazi lililofanya ukaguzi kwa mashirika yote ya serikali kwa lengo la kufutilia mbali yale yasiyo na umuhimu wowote.

Jopo kazi hilo ambalo liliongozwa na mtaalamu wa masuala ya benki Stanley Waudo na aliyekuwa Mbunge wa Mandera ya Kati Abdikadir Mohammed, liliwasilisha ripoti iliyopendekeza mashirika yapunguzwe. Ni pendekezo lilo hilo kutoka IMF ambalo mapema mwaka huu serikali ilikubali kutekeleza ndiposa ipewe mkopo wa Sh255 bilioni. Endapo serikali ingetekeleza pendekezo la jopo kazi hilo la Mbw Waudo na Mohammed, tungekuwa tukivuna matunda ya hatua ambayo Waziri Yatani alitangaza wiki jana.

[email protected]

You can share this post!

WARUI: Nafasi 10,000 za kazi TSC ilitangaza ni chache mno

Modern Coast, Mombasa Raha zasitisha huduma