• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Cristiano Ronaldo aibuka Mfungaji Bora wa Uefa Euro 2020

Cristiano Ronaldo aibuka Mfungaji Bora wa Uefa Euro 2020

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo aliwapiku Harry Kane na Raheem Sterling wa Uingereza pamoja na Patrik Schick wa Jamhuri ya Czech katika vita vya kuwania taji la Mfungaji Bora wa Uefa Euro 2020.

Nyota huyo wa Juventus alifunga jumla ya mabao matano kwenye kipute hicho kilichoshuhudia Ureno waliokuwa mabingwa hao watetezi wakibanduliwa na Ubelgiji kwa kichapo cha 1-0 kwenye hatua ya 16-bora.

Hadi Ureno walipodenguliwa baada ya kusakata mechi nne pekee, Ronaldo alikuwa amepachika wavuni mabao matano na kujiweka pazuri kutwaa kiatu cha dhahabu.

Sogora huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, alifunga penalti mbili katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na Ureno dhidi ya Ufaransa katika mchuano wa mwisho wa Kundi F kwenye Euro mnamo Juni 23. Awali, alikuwa amefunga bao katika kichapo cha 4-2 dhidi ya Ujerumani na kujivunia magoli mengine mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Hungary.

Ufanisi huo wa Ronaldo ulimwezesha kufikia rekodi ya mabao 109 ambayo iliwekwa na Ali Daei wa Iran kati ya mwaka 1993 na 2006. Daei na Ronaldo ndio wanasoka wa pekee wa kiume kuwahi kufunga zaidi ya mabao 90 wakivalia jezi za nchi zao kwenye mapambano ya kimataifa.

Kufikia sasa, Ronaldo tayari ndiye mshikilizi wa rekodi ya mfungaji bora wa muda wote katika soka ya ngazi ya klabu. Aidha, ameibuka mfungaji bora katika soka ya bara Ulaya mara tano.

Wakicheza dhidi ya Ufaransa, Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora katika Kombe la Dunia pamoja na Euro, hivyo kumpiku aliyekuwa fowadi matata wa Ujerumani, Miroslav Klose aliyekuwa akijivunia magoli 19.

Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Euro mnamo Juni 15 wakati ambapo Ureno walikuwa wakicheza na Hungary. Mabao yake kwa sasa kwenye kipute hicho ni 13.

Takriban nusu ya mabao ya Ronaldo yamefungwa katika kipindi cha dakika 30 za mwisho wa mechi. Kufikia sasa, amepachika wavuni magoli 31 katika dakika 15 za mwisho na 22 kati ya dakika 61 na 75 ya mchezo.

Ronaldo amefunga mabao 17 kati ya dakika 16-30 na mara 16 kati ya dakika 31-45. Mabao yake 11 yametokea chini ya dakika 15 za mwanzo wa mechi huku 12 yakifumwa wavuni chini ya dakika 15 za mwanzo wa kipindi cha pili.

Amefunga mabao 89 akiwa ndani ya kijisanduku na 20 mengine akiwa nje ya kijisanduku cha wapinzani. Kati magoli hayo, 14 yametokana na mikwaju ya penalti na tisa mengine yamekuwa zao la mipira ya ikabu au frikiki.

Lithuania na Uswidi ndizo timu ambazo Ronaldo amezifunga mara nyingi zaidi (mabao saba). Hadi kufikia Jumatano usiku katika jiji la Budapest nchini Hungary, hakuwa amefunga bao lolote dhidi ya Ufaransa.

Wanasoka wanaofuata sasa Ronaldo na Daei ni Mokhtar Dahari aliyechezea Malaysia katika miaka ya 70 na 80 na akafunga mabao 89. Wengine ni Ferenc Puskas aliyefungia Hungary mabao 84 kutokana na mechi 85 pamoja na na Godfrey Chitalu aliyefungia Zambia magoli 79 kati ya 1960 na 1980.

Christine Sinclair wa Canada ndiye anashikilia rekodi ya dunia ya ufungaji bora katika soka ya wanawake baada ya kufunga mabao 186 kutokana na mechi 299.

Mabao 109 ambayo Ronaldo amefungia Ureno katika mechi 178 ni rekodi bora ikilinganishwa na magoli 77 ambayo Lionel Messi amefungia Argentina kutokana na michuano 151.

Ina maana kwamba Messi ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 33, anahitaji mabao 23 mingine ili kufikia rekodi ya mabao 100. Kwa kuwa hayo ndiyo magoli amefunga kuanzia 2015, ina maana kwamba atahitaji miaka saba zaidi ili kufikia rekodi ya Ronaldo ya magoli 109.

Ingawa mabao ya Ronaldo yanawiana nay ale yaliyofungwa na Patrik Schick wa Jamhuri ya Czech kwenye Euro mwaka huu, Ronaldo aliibuka kidedea kwa kuwa alichangia goli jingine katika kichapo cha 4-2 walichopokezwa na Ujerumani kwenye Kundi F mnamo Juni 19.

Magoli manne kati ya matano yaliyofungwa na Ronaldo kwenye Euro mwaka huu yalitokana na mikwaju ya penalti.

Alikitia kapuni kiatu cha dhahabu baada ya Kane na Sterling waliopigiwa upatu wa kumbwaga kushindwa kufunga dhidi ya Italia kwenye fainali ya Euro mnamo Jumapili usiku jijini London.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Cha kufanya ili uwe na uso laini na unaong’aa

Mgombea wa ubunge Kiambaa kwa tiketi ya UDA alia serikali...