• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
WANGARI: Ukiritimba ukomeshwe Kenya Power ili kuboresha huduma

WANGARI: Ukiritimba ukomeshwe Kenya Power ili kuboresha huduma

Na MARY WANGARI

KWA muda sasa, Wakenya wamekuwa wakilalamika dhidi ya ukiritimba wa Kampuni ya Kusambaza Umeme Nchini (Kenya Power) ambao kando na kuzorotesha ubora wa utoaji huduma, umewasababishia baadhi yao hasara isiyoambilika.

Licha ya kuwa miongoni mwa kampuni kuu nchini za kiserikali, ambazo bila shaka huwa zimetengewa raslimali zinazohitajika, visa vya umeme kutoweka kiholela katika maeneo mbalimbali nchini vimekuwa kawaida.

Hali hii imewavunja moyo raia ambao wamebaki wakijiuliza maswali tele kuhusu umuhimu wa Kenya Power hasa ni upi?

Katika kisa mojawapo hivi majuzi, mfugaji mmoja wa kuku aliyekata tamaa aligeukia mitandao ya kijamii kuomba ushauri baada ya kupata hasara ya zaidi ya Sh250,000 iliyosababishwa na umeme kupotea ghafla.

Kulingana na mwekezaji huyo chipukizi, alikuwa ndio mwanzo tu ameanzisha biashara ya kufuga kuku wa gredi ambapo alinunua vifaranga, kizimba na lishe wa ndege wake akiwa na matumaini makuu.

Hata hivyo, ndoto yake ilizimwa ghafla wakati umeme ulipotoweka bila kutarajia na kusababisha vifaranga wake wote kufa hali iliyomrejesha sufuri na kumwacha akikadiria hasara kuu.

Mkulima huyo mwenye machungu alitaka kujua ikiwa anaweza kuishtaki Kenya Power ili alipwe fidia hasa wakati huu wa janga la Covid-19 ambalo limelemaza wengi kiuchumi pasipo hata kutaja gharama kuu ya maisha.

Mwekezaji huyo ni mfano tu wa Wakenya wengi wanaozidi kuteseka kutokana na utepetevu wa shirika hilo la kiserikali linalotumia vibaya ukiritimba wake katika usambazaji wa umeme kudhulumu umma.

Vua zianzapo tu kunyesha maeneo mengi nchini hugubikwa na giza totoro baada ya umeme kutoweka hali inayoweza kuendelea kwa siku kadhaa kabla ya kurekebishwa.

Isitoshe, kumekuwa na ripoti za malalamishi kutoka kwa baadhi ya Wakenya ambao wamejipata wakilazimika kulipa bili za juu kupita kiasi za stima.

Wateja wamekuwa wakipigwa na butwaa wanapozabwa na bili za kustaajabisha kila mwisho wa mwezi baada ya mita zao za stima kusomwa na waajiriwa wa Kenya Power.

Licha ya kuanzishwa kwa mfumo mpya, limekuwa suala la kutatanisha kuhusu ni vipi mteja anayetumia stima kwa matumizi ya kawaida nyumbani anaweza kukabidhiwa bili ya hadi Sh50,000.

Wakati umewadia kwa Bunge la Kitaifa kuangazia tena nafasi ya Kenya Power ambayo imezidi kuwanyanyasa Wakenya kupitia ujeuri na utepetevu katika utoaji huduma.

Ni sharti wabunge watekeleze wajibu uliofanya wachaguliwe na wapiga kura kupitia kuunda sheria na sera zitakazolinda raia dhidi ya kunyanyashwa kiuchumi na kupata huduma duni.

Jambo hili litafanikiwa tu kupitia kumaliza ukiritimba wa Kenya Power kwa kufungua sekta ya usambazaji umeme nchini na zaidi kuruhusu ushindani sawia na ilivyofanyika katika sekta ya mawasiliano hali iliyoboresha pakubwa utowaji huduma.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Kaunti ziungane kwa maendeleo

ODONGO: Balaa kwa Jubilee iwapo itapigwa kumbo Kiambaa