• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
ODONGO: Balaa kwa Jubilee iwapo itapigwa kumbo Kiambaa

ODONGO: Balaa kwa Jubilee iwapo itapigwa kumbo Kiambaa

Na CECIL ODONGO

IWAPO chama cha Jubilee kitalemewa katika uchaguzi mdogo wa Kiambaa, Kaunti ya Kiambu hapo Alhamisi wiki hii, basi hilo litakuwa dhihirisho tosha kuwa chama hicho kimekufa na hakitahimili mawimbi makali ya kisiasa kuelekea 2022.

Wapigakura wa eneobunge hilo linalopatikana katika kaunti nyumbani kwa Rais Uhuru Kenyatta, wataelekea debeni Julai 15 kumchagua atakayerithi nafasi ya marehemu Pauli Koinange. Bw Koinange aliaga dunia Machi 31 baada ya kuugua virusi vya corona.

Kuhusu uchaguzi wenyewe, ushindani mkali unatarajiwa kati ya Kariri Njama wa Jubilee na John Njuguna Wanjiku wa UDA, chama kipya kinachovumishwa na Naibu Rais Dkt William Ruto baada ya kuenguliwa nje ya Jubilee.

Baada ya kulambisha Jubilee sakafu kwenye uchaguzi wa mwezi jana eneobunge la Juja, UDA ina hamasa ya kurudia kichapo hicho Kiambaa. Hata hivyo, Jubilee nayo inajikakamua kudhihirisha kwamba umaarufu wake eneo la Kati bado upo imara licha ya wanasiasa wengi kuhamia kambi ya Dkt Ruto.

Mwanzo, kura hii ni muhimu sana kwa Jubilee ambayo pia ilipoteza katika eneobunge la Bonchari ilipobwagwa na ODM mnamo Mei. Katika uchaguzi uliofaa kufanyika Kaunti ya Garissa baada ya kifo cha Yusuf Haji, Jubilee ilinufaika baada ya mwanawe marehemu Abdikadir Yusuf kupewa wadhifa huo kutokana na ukosefu wa mpinzani.

Jubilee inafaa isipoteze kura hiyo, kwa kuwa iwapo haitashinda basi itafuata mkondo wa vyama kama PNU na Narc ambavyo vilitumika na viongozi kuingia ikulu kisha vikasalia vigae baada ya wanasiasa hao kuviasi na kukumbatia vyama vingine.

Rais Mwai Kibaki alitumia Narc ambayo ilikuwa na wanasiasa vigogo kuingia ikulu mnamo 2002 lakini baadaye akawachana na chama hicho baada ya mrengo uliokuwa unawashirikisha Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na William Ole Ntimama kugura na kubuni ODM kuelekea kura ya 2007.

Bw Kibaki alikumbatia PNU ambayo mwisho alitumia kubuni serikali ya nusu mkate na ODM baada ya uchaguzi tata wa 2007 ambao matokeo yake yalisheni ghasia. Kwa sasa vyama vya Narc na PNU ambayo vinara wake ni Gavana wa Kitui Charity Ngilu na Waziri wa Kilimo Peter Munya havina ushawishi wowote wa maana katika siasa za taifa.

Hali hiyo hiyo ilikumba chama cha Kanu ambacho kimekuwa kikifa polepole baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 2002. Kwa sasa Kanu ni kigae cha chama kwa kuwa kina maseneta wawili pekee, wabunge wawakilishi wa wanawake wawili na wabunge sita pekee.

Pili kura hii ni muhimu wakati huu chama hicho kinashiriki mazungumzo na ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Muungano huo utakuwa tu thabiti iwapo kila chama kitaendeleza uthabiti wake katika ngome yake ya kisiasa.

Baada ya kuzuru ikulu wiki jana na Bw Njama kuvishwa kofia na Rais Uhuru Kenyatta, itakuwa aibu zaidi kwa Jubilee kupoteza kiti hicho kwa kuwa kitadhihirisha Rais anaendelea kupoteza udhibiti wa ngome yake kwa Naibu Rais.

Kwa sasa nafasi ni ya wapigakura kumchagua mbunge wao mpya baada ya kampeni za uchaguzi huo kuisha jana. Kuondoa hofu ya ghasia, Mwenyeketi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alizuru eneo hilo wiki jana ambapo aliahidi uchaguzi wenye uwazi mkubwa.

You can share this post!

WANGARI: Ukiritimba ukomeshwe Kenya Power ili kuboresha...

Benitez awaambia Everton wafanye juu chini ili wamsajili...